Na Prince Hoza Matua
MICHUANO ya kombe la NMB Mapinduzi Cup imemalizika siku ya Jumanne iliyopita ambapo miamba Yanga SC na Azam FC zilicheza fainali katika uwanja wa Gombani mjini Pemba.
Yanga SC waliibuka mabingwa wa michuano hiyo kufuatia mikwaju ya penalti 5-3 baada ya sare 0-0 ndani ya dakika 120, golikipa wa Azam FC, Aishi Salum Manula alitokea kuwa gumzo katika mchezo huo baada ya kufanikiwa kuzuia penalti.
Kipa huyo wa zamani wa Simba SC, alizuia penalti iliyopigwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, hata hivyo Manula amekuwa bora katika michuano hiyo kuanzia mchezo wake wa kwanza na mpaka wa mwisho.
Manula amekuwa bora kiasi kwamba watazamaji hawaamini alichonacho, Manula ni zao la Azam FC, kwani Simba SC walimchukua mikononi kwa Azam FC aliyejiunga nayo akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.
Ikumbukwe Manula akiwa Azam FC, alikuwa kipa chaguo la kwanza lakini alikutana na changamoto kadhaa mpaka kumfanya awe kipa wa kwanza kwenye timu hiyo.
Manula alijizolea sifa kemkem kiasi kwamba akabeba Mataji mbalimbali ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu bara, kombe la Mapinduzi na baadaye Klabu Bingwa Afrika mashariki na kati, maarufu kombe la Kagame Cup.
Simba walipoona hawapati mafanikio kwa muda mrefu wakaamua kuvamia Chamazi na kuwakomba nyota wanne wa Azam FC na kuwachukua, nyota hao ni Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, John Bocco na Manula.
Ilikuwa msimu wa 2016/2017 na Simba ilifanikiwa kurejesha ubingwa wa bara, na baada ya hapo Simba ikiwa bingwa wa bara mfululizo na makombe mengine ikiwemo Ngao ya Jamii, Manula aliendelea kuwa kipa chaguo la kwanza ndani ya klabu yake ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.
Ingawa Tanzania ilijaaliwa makipa wengi bora, lakini umahiri wa Manula haukuwa na mfano wake, Manula alikuwa kipa bora kiasi kwamba bara la Afrika lilitokea kumkubali na kumfanya miongoni mwa makipa wa kipekee.
Bahati mbaya Manula aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini jeraha kubwa lililompata hadi kupelekea nafasi yake ya kukaa golini ni lile la kutunguliwa mabao matano na watani wao Yanga.
Katika mchezo wa Ligi Kuu bara, Yanga iliifunga Simba mabao 5-1 ambapo goli la Simba kipa alikuwa Aishi Salum Manula, kipigo hicho hakitasahaulika kamwe kwani Wanasimba wanaamini kwamba kipa Manula alihujumu timu.
Na kuanzia hapo kipa huyo alipoteza namba yake ya kukaa golini, Simba ilifungwa na Yanga bao 5-1 msimu wa 2023/2024 na baada ya hapo Manula hakuonekana tena langoni.
Makocha wote wa Simba hawakumpa nafasi ya kukaa golini nadhani kimaelekezo toka kwa uongozi, na baada ya mkataba kwisha wakaachana naye, Manula akasajiliwa na Azam FC lakini akiwa tayari amepoteza namba ya kudumu.
Katika kikosi cha Azam FC, kocha wa timu hiyo anamtumia Zuberi Foba kama kipa chaguo la kwanza na Issa Fofana kipa chaguo la pili, na Aishi Manula ni kipa chaguo la tatu.
Katika michuano ya kombe la NMB Mapinduzi Cup, kocha Florent Ibenge raia wa DR Congo, amemtumia Manula kama kipa chaguo la kwanza na akafanikiwa kumdhihirisha kwamba yeye ni kipa bora, Manula amewaziba midomo waliomsakama na huenda nafasi yake ya kuwa Tanzania one ikarejea.
ALAMSIKI
