Bao lake dhidi ya Uganda kwenye AFCON 2025 ni la 21 akiwa na Taifa Stars, na kumfanya @smsuva27 kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Msuva ambaye ni zao la akademi ya @azamfcofficial, anampita Mbwana Samatta mwenye mabao 20.
Hapa nazungumzia mabao ya Taifa Stars tu. Mrisho Ngassa anatajwa kama mfungaji bora wa muda wote, lakini sio sahihi.
Kwa Taifa Stars, Ngassa ana mabao kumi tu, ambayo hayamfanyi hata kuwemo kwenye tano bora.
Katika kuhesabu haya mabao kuna kosa kubwa sana hufanyika. Watu huchanganya mabao ya Taifa Stars na ya Kilimanjaro Stars.
Taifa Stars ndio timu ya taifa ya Tanzania, ikijumuisha wachezaji kutoka bara na visiwani.
Hii ndio timu inayoshiriki AFCON, Kombe la Dunia na mechi rasmi za kimataifa.
Kwenye timu hii, Msuva amefunga mabao 21, na ndio anaongoza.
Samatta ana mabao 20, anafuata.
Ngassa ana manao 10.
Halafu Kilimanjaro Stars ni timu ya Bara, ambayo hushiriki CECAFA Senior Challenge Cup pekee.
Kwenye timu hii, Ngassa ana mabao 15, anaongoza. Msuva ana mabao manne na Samatta ana mabao mawili tu.
Kilimanjaro Stars wapinzani wake ni pamoja na Zanzibar. Haiwezekani mfungaji bora wa muda wote wa nchi halafu baadhi ya mabao yake kaifunga nchi hiyo hiyo...ndio hadithi ya Ngassa.
Katika mabao yake 15 ya Kilimanjaro Stars, moja kafunga dhidi ya Zanzibar, mwaka 2009, kwenye CECAFA iliyofanyika Kenya.
Tunapohesabu mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Tanzania, tunaangalia mabao ambayo yamefungwa na Taifa Stars...sio Kilimanjaro Stars.
Na hapa ndipo Simon Msuva anapoongoza. Ngassa anabaki kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Kilimanjaro Stars.
Msuva anakuwa mfungaji bora wa muda wote kwa mabao ya ndani ya miaka 8 tu.
Bao lake la kwanza alifunga Machi 28, 2017 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi.
Stars ilishinda 2-1, bao la pili lilifungwa na Mbaraka Yusuf...la Burundi lilifungwa na Mavugo!
