KOCHA Muargentina, Miguel Angel Gamondi amewarejesha mabeki wakongwe, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Kuwait Ijumaa ya Novemba 14 Uwanja wa Al Salam Jijini Cairo nchini Misri.
Wawili hao hawakuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichochapwa 2-0 na Iran Oktoba 14 kwenye mchezo mwingine wa kirafiki Uwanja wa Rashid, Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) chini ya kocha mzawa, Hemed Suleiman Ali ‘Morocco’ aliyeondolewa baada ya kichapo hicho.
TFF ilimtambulisha rasmi Gamondi November 4 kuwa kocha mpya wa Taifa Stars baada ya makubaliano na klabu yake, Singida Black Stars na kikosi chake kinatarajiwa kuingia kambini Jumapili baada ya mechi za wikiendi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara tayari kwa safari ya Misri.
