Na Prince Hoza Matua
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemtambulisha Muargentina Miguel Angel Gamondi kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya wakubwa ‘Taifa Stars’ baada ya kuachana na mzawa, Hemed Suleiman Ali ‘Morocco’.
Gamondi ataiongoza Tanzania kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Kuwait Ijumaa ya Novemba 14 Uwanja wa Al Salam Jijini Cairo nchini Misri.
Ni wiki kocha huyo wa Singida Black Stars alipotangazwa kuwa kocha mpya wa Taifa Stars akichukua nafasi ya mzawa, Hemed Suleiman Ali ‘Morocco’ aliyeondolewa.
Gamondi amekitaja kikosi chake kwa ajili ya mchezo huo baada ya mechi za wikiendi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara tayari kwa safari ya Misri.
TFF imechukua hatua hiyo ya kumfuta kazi Morocco na kumwajiri Gamondi ambaye mafanikio yake akiwa na klabu ya Yanga SC pamoja na Singida Black Stars tunayafahamu.
Kocha huyo kipenzi cha wengi alijiunga na Yanga msimu juzi akichukua mikoba ya Nasreddine Nabi raia wa Tunisia ambaye naye aliiwezesha Yanga kufika fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya Yanga kufika hatua hiyo ya fainali, Nabi aliamua kuachana na timu hiyo na kutimkia klabu ya FAR Rabat ya Morocco, mbali na kuwafikisha Yanga fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bara na kombe la FA huku pia ikibeba Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu.
Alipoondoka Nabi, uongozi wa Yanga ulimtambulisha Muargentina huyo ambaye alikwenda kuibadili zaidi Yanga na kuwa miongoni mwa timu tishio barani Afrika, ikiwa na Gamondi Yanga iligeuka mbabe kwa mtani wake Simba, ikianza kwa kuifunga Simba mabao 5-1.
Gamondi akiwa na Yanga iliweza kuifunga Simba mara nne mfululizo kabla ya makocha wenzake wawili Miloud Hamdi raia wa Algeria na Ramon Folz raia wa Ufaransa kuendeleza vipigo kwa Simba na kuwa mara sita mfululizo.
Lakini pia Gamondi aliiwezesha Yanga kutetea mataji yake ya ndani yaani Ligi Kuu bara, kombe la FA na Ngao ya Jamii, vile vile Yanga ilifanikiwa kwa mara ya kwanza kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika baada ya mwaka 1998.
Mpira wa Gamondi hakuna shabiki wa soka hapa nchini ambaye haujuwi, Yanga ya Gamondi ilikuwa inasifika kwa soka lake la kushambulia kwa kasi kiasi kwamba timu mbalimbali hasa zile zenye majina makubwa kama Mamelodi Sundown's ya Afrika Kusini au CR Belouizdad ya Algeria zilikutana na moto wake.
Yanga ya Gamondi iliogopeka mpaka pale alipoanza kuhujumiwa na baadaye akaondoka nchini, Singida Black Stars ilimrejesha tena Tanzania na kumpa jukumu la kuinoa timu yake ilianza kushiriki kombe la Klabu bingwa Afrika mashariki na kati, (Kagame Cup).
Kocha huyo aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa, na sasa ameiwezesha kutinga hatua ya makundi kombe la Shirikisho Afrika, maamuzi ya TFF kumpa kibarua cha kuinoa Taifa Stars ambayo baadaye itakwenda kushiriki fainali za AFCON zitakazofanyika Morocco.
Nina imani na Gamondi kwenye fainali za AFCON na mashindano mengine ambapo Stars itakwenda kushiriki, Gamondi ni kocha wa misheni, hivyo tutegemee makubwa kutoka kwake, Stars ilihitaji kocha aina ya Gamondi muda mrefu isipokuwa mamlaka ilikuwa inapuuza maoni ya wadau.
Naishukuru TFF kwa kusikiliza maoni ya wadau wakianza na wale waliokuwa wanataka kocha Hemed Morocco afutwe kazi, Morocco hakupaswa kuendelea kuinoa timu hiyo kwani kwa ukubwa wa Stars ilihitaji kocha mwenye uwezo mkubwa.
Gamondi ni kocha wa misheni hivyo wachezaji sasa wanatakiwa kutimiza malengo, bilioni vya Watanzania kwa timu ya taifa vilikuwa kwa kocha ambaye alishindwa kuwaunganisha ndani ya uwanja, Gamondi anajua kuunganisha wachezaji na haitachukua muda mrefu timu yetu itapata mafanikio.
ALAMSIki