MABINGWA wa Tanzania, Yanga wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wiliete SC ya Angola katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC katika mchezo huo yamefungwa na viungo, Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 70 na mzawa, Aziz Andambwile Mwambalaswa dakika ya 86.
Kwa ushindi huo, Yanga inaitupa nje timu hiyo ya Benguela kwa jumla ya mabao 5-0 kufuatia ushindi wa ugenini wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Novemba 11, Jijini Luanda nchini Angola, mabao ya Andambwile dakika ya 31, kiungo mwingine Edmund Godfrey John dakika ya 71 na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo dakika ya 79.
Sasa Yanga itakutana na Silver Strikers ya Malawi ambayo imeitoa ASSM Elgeco Plus ya Madagascar kwa mabao ya ugenini leo ikitoa sare ya 0-0 Uwanja wa Taifa wa Bingu Jijini Lilongwe kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza ugenini.