WENYEJI, Tanzania Prisons wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji Oscar Mwajanga Mwasanga dakika ya 14 ya mchezo huo, huo ukiwa ushindi wa kwanza kwa Tanzania Prisons baada ya mechi tatu tangu kuanza kwa msimu huu.
Mechi mbili za awali Tanzania Prisons ilifungwa 1-0 mfululizo ugenini dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Namungo FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Kwa upande wao KMC wanapoteza mechi ya pili kati ya tatu, nyingine wakifungwa pia 1-0 na Singida Black Stars baada ya kushinda 1-0 na wao katika mchezo wa kwanza dhidi ya Dodoma Jiji mechi zote wakicheza nyumbani Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.