TIMU ya Simba SC imefanikiwa kuingia Hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya sare ya kufungana bao 1-1 na Gaborone United ya Botswana katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza leo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mabao yote yalipatikana kwa mikwaju ya penalti, Simba SC wakitangulia kupitia kwa kiungo mshambuliaji Muivory Coast, Jean Charles Ahoua dakika ya 45, kabla ya kiungo mwingine mshambuliaji wa Kimataifa wa Botswana, f Lebogang Ditsele kuisawazishia Gaborone United dakika ya 58.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Obed Itani Chilume, zamani Francistown Sports Complex mjini Francistown, Botswana – bao la winga wa Mkongo, Elie Mpanzu Kibisawala dakika ya 16.
Simba SC sasa itakutana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini ambayo imeitoa Simba Bhora ya Zimbabwe kwa penalti 4-2 baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 mchezo mmoja.