TIMU ya Azam FC imefanikiwa kwenda Hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na beki wa Kimataifa wa Mali, Yoro Mamadou Diaby dakika ya 18 na kiungo mshambuliaji, Nassor Saadun Hamoud dakika ya 90’+2.
Kwa matokeo hayo, Azam FC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-0 kufuatia kuichapa Al Merreikh Bentiu 2-0 pia kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Juba Jijini Juba, Sudan Kusini.
Kwenye mchezo huo, mabao ya Azam FC yalifungwa na kiungo wa Kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum Abdallah dakika ya 23 na mshambuliaji mpya Mkongo, Bola Jephte Kitambala dakika ya 70.
Azam FC saaa itakutana na KMKM ya Zanzibar ambayo imeitoa AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2 ikishinda 2-1 kila mechi zote zikipigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.