Na Prince Hoza
NAWAPA hongera Wekundu wa Msimhazi, Simba SC kwa kufanikiwa kuingia fainali ya kwanza ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.
Simba imeingia fainali baada ya kuiondosha timu ya Stellanboch ya Afrika Kusini kwa jumla ya bao 1-0, ilipata ushindi jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Mkapa, na mwishoni mwa wiki iliyopita ikilazimishwa sare tasa 0-0 uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban nchini Afrika Kusini.
Hii ni fainali yake ya kwanza kwa Wekundu hao wa Msimhazi, lakini ni fainali yake ya pili katika historia ya klabu hiyo tangia ilipoanzishwa mwaka 1935, mwaka 1993 Simba iliingia fainali ya michuano ya kombe la CAF.
Shirikisho la soka barani Afrika lilikuwa na michuano yake mitatu ya ngazi ya vilabu, Klabu Bingwa Afrika ambapo mabingwa wa nchi husika barani humu hushiriki michuano hiyo, na kombe la Washindi ambapo wanaoshika nafasi ya pili nao hushiriki michuano hiyo.
Lakini Shirikisho hilo liliamua kuanzisha michuano mingine ambayo wanaoshika nafasi ya tatu nao hushiriki, lakini pia nchi zilianzisha michuano ya ndani ya vilabu kama kombe la FA ambapo Bingwa alipata nafasi ya kushiriki michuano mipya ambayo iliitwa kombe la CAF.
Na mwaka 1993 klabu ya Simba ya Tanzania ikiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye Ligi ya nchi, ilipata nafasi ya kushiriki michuano hiyo, Wekundu hao walifanikiwa kufika fainali ambapo ilijikuta inakutana na mwakilishi wa Ivory Coast Stella Abdijan na kufungwa mabao 2-0 na kombe lilienda Ivory Coast.
Sitaki kuyakumbusha ya 1993 kwani yaliwaumiza wengi akiwemo aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Mwinyi ambaye sasa ni marehemu.
Rais Mwinyi alidiriki kusema Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu kwa sababu Simba ilikubali kichapo klcha mabao 2-0 kwenye ardhi ya nyumbani, Simba ilianzia ugenini na ikiilazimisha Stella Abdijan kwenda nayo sare tasa 0-0.
Kipigo Cha mabao 2-0 kiliwaumiza wengi na ikikosa zawadi ya magari aina ya KIA ambapo mfadhili wa zamani wa klabu hiyo Azim Dewji aliahidi kuwapa kila mchezaji endapo Simba itachukua ubingwa.
Simba ikikosa taji hilo mwaka 1993 kabla ya Shirikisho la soka Afrika, CAF kuyaunganisha michuano hiyo na kombe la Washindi na hatimaye kuwa kombe la Shirikisho mwaka 2004 na Simba kufanikiwa tena kuingia fainali mwaka huu 2025.
Kikosi cha Simba msimu huu na kocha wake Fadlu David's raia wa Afrika Kusini wataingia kwenye rekodi za kudumu za klabu hiyo, niwape pongezi sana Simba kwa kuweza kuandikisha historia hiyo ambayo inaweza kudumu kwa vipindi na vipindi.
Naamini mpira wetu umepiga hatua kiasi kwamba vilabu vyetu vinaweza kurudia mafanikio yake kwa msimu na msimu, lakini kitendo cha Simba kufika fainali kinahitaji salamu za pongezi
kutoka kwa kila Mtanzania.
Yanga SC msimu juzi 2023 walikuwa wa kwanza kuandika rekodi ya kuwa timu ya Tanzania kufika fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika na ilicheza na timu ya USM Alger ya Algeria.
Simba nao watacheza na RSB Berkane ya Morocco na ikifanikiwa kuijibu rekodi ya Yanga, ingawa Simba inaweka rekodi nyingine ya kuwa timu ya kwanza nchini kuingia fainali ya pili ya CAF
Wachezaji wa Simba waliopo kwenye cha sasa wanastaili kila aina ya pongezi kwani watakumbukwa katika kipindi chao chote kama kilivyoimbwa kikosi kilichoingia fainali ya kombe la CAF mwaka 1993 ama wa enzi za mwaka 1974 ambapo kilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika.
ALAMSIKI
