SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya ghafla ya Mwamuzi wa mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Stellenbosch ya Afrika Kusini dhidi ya Simba Sc utakaochezwa Jumapili, Aprili 27, 2025.
CAF imempanga Mwamuzi Maarouf Eid Mansour kutoka Misri akichukua nafasi ya Amin Omar naye kutoka Misri ambaye awali alipangwa kuchezesha mechi hiyo ingawa haijafahamika sababu za mabadiliko hayo ya ghafla.
Mwamuzi Mansour atasaidiwa na wenzake kutoka Misri ambao ni Mahmoud Abouelregal na Ahmed lbrahim ambao tangu awali walipangwa kwa wasaidizi lakini pia kuna mabadiliko kwa refa wa akiba ambapo sasa atakuwa Mahmoud Nagy naye kutoka Misri.
Bechir Hassani kutona Tunisia atakuwa Mtathmini wa marefa huku Kamishina wa mechi hiyo akiwa Kelesitse Gilika wa Botswana. Hakuna mabadiliko upande wa marefa wanaosimamia teknolojia ya video ya usimamizi kwa marefa (VAR) ambapo kuna Mahmoud Ashour na Mahmoud Elbana wote kutoka Misri.
Hatua ya CAF kufanya mabadiliko hayo ni faraja kwa wafuasi wa Simba Sc huku Amin Omar akitajwa kuwa Mwamuzi mwenye historia mbaya na Wekundu hao wa Msimbazi.
Itakumbukwa refa huyo ndiye alichezesha mechi ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Horoya katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2022/2023.
