Kocha Mkuu wa Tabora United, Genesis Mangombe ameachia ngazi rasmi akiwa sambamba na msaidizi wake baada ya kutofurahishwa na mwenendo wa timu. Vyanzo vinaeleza Mangombe "amekosa hamasa ya kuendelea na safari ya mateso."
Kwa sasa, timu ipo chini ya Kocha Msaidizi Khalfan Mbonde, ambaye anashikilia jahazi lililopigwa mawimbi kabla ya safari ya kwenda Singida.
Hali haijawa shwari pia kwa upande wa uongozi CEO Charles Obien, raia wa Kenya, naye amepunguza kasi, akidai "lipeni niondoke kwa heshima", huku akikwepa mikiki ya ligi kuu kama mchezaji aliyepigwa kanzu mara tatu mfululizo.
Jumamosi hii, April 19, Tabora United itashuka dimbani dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Liti, Singida. Mchezo huo utaongozwa na Kocha Mbonde, ambaye kwa sasa ana jukumu la kuzuia jahazi lizamie kabla halijafika mtoni.
Mashabiki wa Tabora United sasa wanasema, "Timu imekuwa kama gari bila dereva, ila matumaini bado yapo... tukipata draw itakuwa kama ushindi wa Kombe la Dunia!"
