ANGUKO LA YANGA LINAKUJA.......

NA PRINCE HOZA

LICHA kwamba rekodi zinaendelea kuandikwa, lakini kadri siku zinavyozidi kusogea ndipo linapoonekana anguko la Yanga, hata Simba ilionekana hivi hivi na sasa imekuwa ni kawaida Simba kuwaona kwenye nafasi ya tatu au ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Yanga inaelekea kuanguka ingawa  kwasasa ipo kileleni inaongoza Ligi Kuu Tanzania bara inayodhaminiwa na benki ya NBC, Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 24 ikicheza mechi 8 na haijapoteza mchezo wowote wala haijaruhusu bao lolote.

Ukiangalia rekodi zake za msimu unaweza kudhani ni kubwa kuliko za msimu uliopita kwani rekodi ya msimu uliopita ikicheza mechi saba za mwanzo tayari ilishapoteza mchezo mmoja dhidi ya Ihefu SC ya Mbalali mkoani Mbeya.

Lakini pia rekodi za msimu uliopita kwenye ligi hiyo Yanga iliruhusu zaidi ya goli moja, tofauti na msimu huu ambapo mpaka imefikisha mechi 8 bado haijaruhusu bao lolote na ikishinda mechi zote.

Msimu uliopita Yanga SC ilikuwa moto wa kuotea mbali na ikifanikiwa kushinda mataji mawili makubwa, Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu bara na pia ilitwaa kombe la CRDB Cup, Yanga pia ilifika robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Licha ya rekodi hizo, Yanga iliwaacha hoi pale ilipokuwa ikiibuka na ushindi mkubwa katika michezo yake ya nyumbani, ilianza ligi kwa kishindo kwa kuifunga JKT Tanzania mabao 5-0, lakini ikizichapa KMC na Simba SC mabao 5-0 kila mmoja.

Vipigo vya mabao matano viliendelea kwa kila aliyekatiza mbele yake, falsafa ya uchezaji wa kikosi kinachonolewa na Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina kiliwafurahisha mashabiki wa timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani.

Miguel Gamondi kocha wa Yanga

ANGUKO LA YANGA

Kuna dalili zote Yanga SC inakwenda kuanguka, huenda si leo wala kesho ila Yanga inaenda kuanguka, samahani sana wapenzi wasomaji wa makala yangu ya MIKASI mnielewe kuwa Yanga inaenda kuanguka.

Hakuna hata mmoja anayepanda kwenye kilele cha mlima anabaki huko huko, kuna siku atashuka, anguko la Yanga linakuja pale timu yao itakapopoteza mchezo wao ligi, anguko lingine kwa Yanga ni pale itakaoovuliwa na ubingwa wa bara.

Yanga inaweza kuvuliwa ubingwa endapo washindani wake watakapopata dawa ya kumfunga, Yanga inaweza kufungwa wakati wowote kuanzia sasa kwani mwenendo wake si mzuri.

Kutoka kwenye ushindi wa mabao matano matano ya msimu uliopita na soka la kuvutia lenye kasi mithili ya farasi au swala iliwaacha hoi Simba na Azam ambao walisubiri nyuma yake wakiachwa kwa alama nyingi.


Hata msimu huu mwanzoni mwa Ligi Kuu bara Yanga imewaacha nyuma Simba na Azam, mshindani wake kwenye ligi hiyo ni Singida Black Stars, lakini ligi bado sana kwani mzunguko wa pili haujafika na lolote linaweza kutokea.

Anguko lingine la Yanga ni pale viwango vya wachezaji wake kushuka, kwa mfano kiwango cha top score wa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu bara Stephanie Aziz Ki si cha kuridhisha, Aziz Ki msimu uliopita alifunga mabao 21 na kuwa mfungaji bora lakini sasa ana bao moja tu.

Hata viwango vya nyota wengine wa Yanga kama Khalid Aucho, Pacome Zouzoua, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Kouassi Attoholoa Yao "Jeshi", Prince Dube vimeshuka ghafla, sijui tatizo ni nini! Lakini kwa mwenendo huu kuna uwezekano wa Yanga kupoteza mechi na ikajikuta ikiandamwa na vioigo.

Hilo linaweza kuwakuta kwani ushindi wao umekuwa mdogo, Yanga ikishinda bao 1-0 tena ikizifunga timu ndogo na dhaifu, hata Simba ambao msimu uliopita waliwafunga 5-0, lakini walipokutana tena Yanga ilishinda 1-0 tena goli la kujifunga wenyewe, ambapo beki wa pembeni Kelvin Kijili alijifunga kwa bahati mbaya.

Ushauri wangu kwa Yanga ili waendelee kuwa wafalme wa soka la Tanzania itabidi wafanye usajili kabambe kwani kuna baadhi ya wachezaji wanaonekana kupoteza uwezo wao, lakini kingine sifa zimewajaa na wanajiona wako safi kumbe wapinzani wao wamewasoma mbinu zao na sasa wanashindwa kuja na mbinu mpya....
ALAMSIKI


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA