MWINYI KUTILIA MKAZO UJENZI WA VIWANJA VYA MICHEZO
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya nane inatilia mkazo ujenzi wa viwanja vya michezo mbalimbali ili kutanua wigo wa ajira kutokana na michezo pamoja na kuibua vipaji vya vijana.
Amesema azma ya Serikali ni kuendeleza michezo katika nyanja zote inatimia kwa kuweka miundombinu ya kisasa iliyobora na imara.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipoufungua Viwanja vya Michezo Matumbaku Sports Complex uliopo Shehia ya Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar tarehe: 30 Disemba 2023.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi amewatoa hofu wananchi wa Malindi kuwa dhamira ya ujenzi wa viwanja hivi ni kuwa mbadala maeneo yaliyofanyiwa uwekezaji.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amewataka vijana watumie fursa za kuwepo kwa viwanja vipya vya kisasa kwa kuonyesha vipaji vyao ili waweze kutengeneza ajira ndani ya nchi na nje.
Pia amesema michezo ikitumika vizuri itakuwa ni fursa ya kuitangaza Zanzibar na kukuza utalii.
Eneo hilo lina viwanja vitatu vya mpira wa miguu, pamoja na kiwanja kimoja kwa michezo ikiwemo mpira wa wavu, mpira wa kikapu na netiboli.