HONGERA TABIA BATAMWANYA KWA KUSHINDA TUZO
Na Prince Hoza
HONGERA sana tena sana mwanadada Tabia Batamwanya kwa kushinda tuzo ya mwimbaji bora wa muziki wa dansi ilitolewa hivi karibuni, haikuwa rahisi kwa mwanadada huyo kubeba tuzo hiyo kwani ameipigania kwa muda mrefu sana.
Batamwanya ni msanii wa siku nyingi lakini jina lake limeanza kufahamika hivi karibuni kutokana na kuvuma kwa wimbo wake wa "Narudi nyumbani" aliomshirikisha mwanamuziki wa bongofleva Uncle Some.
Batamwanya alianza kujulikana tangu mwaka 2006 pale alipojikita kwenye sanaa ya ulimbwende, msanii huyo aliibuka mshindi wa Miss Singida na kufanikiwa kushiriki mashindano ya Miss Tanzania.
Ikumbukwe Batamwanya alishiriki sambamba na Wema Sepetu ambaye aliibuka mshindi na kuwakilisha Tanzania kwenye Miss World, safari ya Batamwanya kwenye urembo nadhani iliishia hapo na alijikita kwenye muziki wa dansi.
Batamwanya ni mtoto wa mwanamuziki wa zamani wa muziki wa dansi nchini Jumbe Batamwanya ambaye alihudumu katika bendi ya Bima Lee Orchestra ambapo alijipatia umaarufu mkubwa.
Historia ya Jumbe Batamwanya aliyetamba na wimbo uitwao "Siri" alipendelea kuambatana steji na mtoto wake wa kike ambaye ndiye huyu Tabia Batamwanya na ilitabiriwa kwamba atakuja kumrithi baba yake miaka ya baadaye atakapokuwa mkubwa.
Kwasasa Jumbe Batamwanya ametangulia mbele ya haki na Tabia akaamua kumrithi baba yake, kwa bahati mbaya sana Tabia aliangaika bila mafanikio kwani alishiriki kutumikia bendi mbalimbali na kuambulia msoto.
Mimi binafsi niliwahi kukutana na Tabia ambaye maskani yake ni Manzese Mkunguni jijini Dar es Salaam, alionyesha kutata tamaa kwani muziki wa dansi haukumlipa, Tabia anasema baba yake alipata mafanikio makubwa enzi zake ikiwemo kujenga nyumba ya kuishi na kununua gari.
Baba yake alifanikiwa kupata ajira katika shirika la Bima na kwakifupi
alijipatia umaarufu mkubwa, lakini yeye alitaabika na aliona umuhimu wa kuacha muziki wa dansi.
Kuna wakati alijikita kwenye uigizaji na baadaye akajifunza utangazaji na alihudumu kwenye tv online, binafsi namfahamu vizuri Tabia Batamwanya.
Lakini sasa amegeuka malkia wa muziki wa dansi hapa nchini, jina la Tabia Batamwanya ndio gumzo kwasasa kwani wimbo wake wa "Narudi nyumbani" imemtambulisha vema, mwanadada huyo akaingia kwenye Top ten za redio mbalimbali hapa nchini.
Pia staa huyo wa muziki wa dansi akaingia kwenye kuwania tuzo zinazowahusisha wanamuziki wa dansi, nimeamua kumpa hongera kwani tuzo hiyo itamuongezea ari na kasi mpya na kumrejeshea morali ya kuupenda muziki.
Tayari bendi mbalimbali kubwa hapa nchini zilianza kumuwania ikiwemo Msondo Ngoma, Sikinde Ngoma ya Ukae, lakini Ally Choki kupitia bendi yake ya Extra Bongo wana Next Level imefanikiwa kumchukua na sasa anaitumikia bendi hiyo.
Tabia Batamwanya anaanza kuhesabu tuzo na akianza na hii ya Cheza Kidansi Awards na baadaye Kilimanjaro Tanzania Music Awards.
ALAMSIKI