SIMBA NA YANGA LEO NANI ATALALA MAPEMA!
Na Saida Salum. Dar es Salaam
Leo ndio leo asiyekuwa na mwana abebe jiwe ndivyo msemo wa kiswahili unavyoweza kutumika wakati watani wa jadi wa soka la Tanzania, Simba Sc na Yanga Sc watakapoumana jioni ya leo uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Katika kuelekea mchezo huo, Simba wanaonekana wako vizuri kuliko mahasimu wao Yanga ambao mashabiki wake wanaonekana wameikatia tamaa timu yao kutokana na matokeo wanayoyapata kwenye ligi, lakini kwa mujibu wa historia za timu hizo zinapokutana timu inayokuwa imeenea huwa inafungwa na ile inayoonekana dhaifu.
Yanga inaingia uwanjani bila ya kocha wao mkuu, Mzambia George Lwandamina ambaye ameacha kazi na kurejea kwao Zambia na kuna taarifa amejiunga na timu yake ya zamani ya Zesco United, pia inaendelea kuwakosa nyota wake muhimu washambuliaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe jambo ambalo linawanyima imani mashabiki wake huku sasa ikipanga kuwategemea Obrey Chirwa, Raphael Daudi, Yusuph Mhilu na Ibrahim Ajibu.
Wakati Simba yenyewe inatambia washambuliaji wake wachana nyavu Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi na John Raphael Bocco ambao wameifanya timu hiyo msimu huu kuwa kileleni kwa wingi wa pointi ambazo ni 59 zikiwaacha nyuma sana wapinzani wake kwani Azam Fc wanaoshika nafasi ya pili wana pointi 49 na Yanga inayoshika nafasi ya tatu ina pointi 48.
Yote kwa yote sijui nani atalala mapema leo, timu hizo zote ziliweka kambi mjini Morogoro na kila moja katika mechi zake za ligi Simba ikicheza na Lipuli Fc ilitoka sare ya 1-1 wakati Yanga nao wakacheza na Mbeya City wakatoka sare pia ya 1-1, mgeni rasmi katika mchezo wa leo ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Poul Makonda