Njombe Mji yajinasua mkiani, Mbeya City nayo yabanwa
Na Mwandishi Wetu. Njombe
Timu ya soka ya Njombe Mji ya mjini Njombe jioni ya leo imeutumia vema uwanja wa nyumbani baada ya kuilaza Ndanda Fc ya Mtwara mabao 2-0 uwanja wa Sabasaba mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Vijana wa Njombe Mji wakicheza mbele ya mashabiki wao wameweza kutakata kwa mabao hayo mawili yaliyowekwa kimiani na Notikeli Masasi na Ahmed Adwale na kuifanya timu hiyo kupanda kwa nafasi moja ikitoka nafasi ya 16 hadi ya 15 huku Majimaji Fc ya Songea sasa ikishikilia mkia, Njombe Mji iliyocheza mechi 25 imefikisha pointi 20.
Nayo Singida United imenusurika kichapo toka kwa Mbeya City baada ya kulazimisha sare na wenyeji wao uwanja wa Sokoine mjini Mbeya jioni ya leo.
Mbeya City walitangulia kupata bao lililofungwa na beki wake Haruna Shamte kabla ya Maliki Antiri kuisawazishia Singida United inayonolewa na Mholanzi, Hans Van der Pluijm
Ligi hiyo inaendelea tena kesho kwa timu ya Majimaji ya Songea na Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar dhidi ya Azam Fc na Stand United dhidi ya Kagera Sugar