KISPOTI

SIMBA KUMTOA MO IBRAHIM KWA MKOPO NI JAMBO LA BUSARA SANA

Na Prince Hoza

SIMBA SC na Yanga Sc zinaumana Jumapili ijayo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hiyo ni mechi kubwa hapa nchini ambapo wapenda soka watajitokeza kushuhudia mtanange huo.

Lakini jina la Mo Ibrahim halimo katika kurasa za magazeti ya michezo hasa ya hapa nchini, Mo Ibrahim ni mchezaji wa Simba Sc ambao kwa sasa wanaongoza ligi, Simba wapo kileleni kwa pointi zao 59 wakiiacha nyuma ya pointi 11 mtani wake Yanga Sc.

Kikosi cha kwanza cha Simba hata mtoto mdogo ukimpa akupangie atakutajia kuanzia mlinda mlango hadi winga wa kucheza namba 11, na pia atakutajia wachezaji wanaokaa benchi, kwa vyovyote Mohamed Ibrahim "Mo" atakuwa jukwaani akiufuatilia mpira huo.

Siku nyingi sana sijamuona Mo Ibrahim akiwa ameuvalia ule uzi wa rangi nyekundu na micharazo meupe mabegani, Mo sijamuona hata benchi akisubiri kuchukua nafasi aingie, tayari mashabiki wameshamsahau.

Ilikuwa ngumu mashabiki wa Simba kumsahau Jonas Mkude, walipiga ukelele kwa kocha wao Mcameroon, Joseph Omog, na walipoona hampi sana nafasi Mkude wakamchongea kwa viongozi na mwishowe akaletewa msaidizi Mrundi Masoud Djuma Irambona kisha baadaye akafutwa kazi mazima.

Mashabiki wa Simba walimpenda sana Mkude kuliko kocha Omog na ndio maana alipotimuliwa Omog furaha iliongezeka, walijua mchezaji wao wanayempenda atacheza, hivyo ndivyo ilivyo kwa Mohamed Ibrahim "Mo" naye alihusudiwa na mashabiki wa Simba.

Lakini kwa sasa mashabiki hao hao wa Simba wametulia na hawapigi tena kelele za kumtaka Mo acheze, na ndio maana iko kimya sana sauti ya kumtaka Mo acheze, na ukimya wake umezidi kumpoteza kabisa kisoka.

Hakuna mtu anayemtaka Mo kwa sasa, na wanaelekea kwenye mchezo wao na Yanga Mo hayumo wala hazungumzwi, maisha yanakuwa magumu sana kwake, lakini kabla hajaongezewa mkataba na Simba, taarifa za kutakiwa na mahasimu Yanga zilisambaa.

Inasemekana Yanga walikuwa wakimuhitaji kwa udi na uvumba, Mo bado ni mchezaji mzuri na kama anapewa nafasi basi anaweza kuonyesha vitu vyake, lakini kwa ubora unaoonyeshwa na wachezaji wa Simba sidhani kama kuna namba yake.

Kocha mkuu wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre na msaidizi wake Masoud Djuma Irambona nawaona wako sahihi na kikosi chao, hawana upendeleo wowote kwa wachezaji wao, wanawapanga kutokana na kile qanachokifanya uwanjani, na ndio maana Simba inaongoza ligi.

Wekundu wa Msimbazi wanaongoza ligi wakiwa na pointi 59 na mechi 25 wakifuatiwa na Yanga Sc wenye pointi 47 na mechi 23, isipokuwa Yanga ana mechi zake mbili za viporo hajacheza kwa maana hiyo kama akicheza na kushinda anaweza kubakiza gepu la pointi 5 hivyo Jumapili itakuwa mechi ngumu.

Simba watacheza kwa jihadi na wakiingia uwanjani kwa kutegemea kikosi chao cha kwanza ambapo Mo Ibrahim hatokuwepo, Dirisha la usajili litagunguliwa tena Juni mwaka huu hasa baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu bara msimu wa 2017/18.

Hivyo wachezaji ambao mikataba yao inamalizika na hawana msaada wanaachwa waende kwingineko, na wale ambao mikataba yao bado haijakwisha na hawana msaada wanatolewa kwa mkopo, msaada wa Mo Ibrahim ndani ya Simba kwa sasa siuoni kabisa hivyo itakuwa jambo la busara kama viongozi wa Simba na benchi zima la ufundi wakamtoa kwa mkopo nyota huyo ili akaonyeshe kiwango chake kwingineko.

Mwisho namalizia kuwa Mo Ibrahim ni hazina ya taifa hivyo kama atakuwa anacheza katika kiwango chake kilekile tulichomzoeaga kuanzia Mtibwa Sugar na Simba Sc bila shaka ataitwa na timu ya taifa, Taifa Stars na kuisaidia nchi yetu

Alamsiki

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA