Kispoti;
Mayanga kosa lake liko wapi! asihukumiwe
Na Prince Hoza
KELELE zimekuwa nyingi mno kutoka kwa wadau na mashabiki wa soka zikimsakama kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Shaaban Mayanga.
Kelele hizo nyingine zikimtaka ajiweke kando kuinoa timu hiyo, yote yanakuja kufuatia timu hiyo ya taifa kuchapwa mabao 4-1 na Algeria mchezo wa kirafiki unaotambuliwa na Shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa).
Mchezo huo ulifanyika nchini Algeria, hivyo timu hiyo ilisafiri kutoka Dar es Salaam hadi mjini Algiers kuwafuata Mbweha hao wa Jangwani, Stars iliingia kambini mapema juma lililopita kujiandaa na mechi mbili za kirafiki za kimataifa.
Mchezo mwingine wa kirafiki unachezwa leo katika uwanja wa Taifa dhidi ya DR Congo, hivyo baada ya kupoteza ugenini kwa mabao hayo 4-1 Watanzania wameona tatizo lipo kwa kocha Mayanga.
Kumlaumu kocha huyo hasa kwa kufungwa na Algeria sidhani kama kuna weledi umetumika wa kutosha katika kuutathimini mchezo huo dhidi ya timu kubwa ya Algeria, wenzetu wa Afrika ya kaskazini tukubali tu kuwa wapo juu zaidi yetu kisoka.
Soka la Afrika, sehemu kubwa linabebwa na Afrika kaskazini na hilo halina ubishi, ligi yao inaongoza kwa ubora barani Afrika na wachezaji wanaounda kikosi kizima cha timu zao za taifa karibu wote wanacheza katika ligi kubwa kubwa duniani.
Wakati sisi Tanzania tuna mchezaji mmoja tu Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa kwenye ligi kubwa duniani, Samatta anacheza katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Wengine waliosalia wote wanacheza barani Afrika, Simon Msuva mfungaji wa goli la Tanzania katika mchezo huo, yeye anacheza soka la kulipwa nchini Morocco katika klabu ya Difaa Hassan El Jadida inayoshiriki Ligi ya mabingwa barani Afrika.
Rashid Mandawa ambaye hakuaminiwa sana na kocha wa Stars, yeye anacheza nchini Botswana katika klabu ya BDX inayoshiriki Ligi Kuu na Abdi Banda naye anacheza nchini Afrika Kusini, wengine wote waliobaki wanacheza katika ligi ya Tanzania ambako soka lake lipo chini mno.
Hiki siyo kipindi cha kumlaumu Mayanga ambaye ameiongoza timu hiyo kucheza mechi 16 ikipoteza mbili tu na nyingine kushinda na kutoka sare, Awali wadau wa soka nikiwemo mimi tulihoji Taifa Stars kucheza mechi za kirafiki nyumbani tena na timu zilezile za levo yake.
Tulilalamika sana Stars kucheza na Malawi kila mara katika mechi za kirafiki za Fifa, mawazo yetu yakasikika na Stars ikaanza kucheza na timu zilizo juu yetu tena ugenini.
Na unapoenda kucheza ugenini tena na timu zilizotuzidi kiwango usitegemee kupata ushindi, mechi kama zile zinawasaidia wachezaji wetu kuongeza uzoefu na kuzoea mechi kubwa kitu kinachopelekea faida hasa anapokutana na timu nyingine iliyo chini yetu ama juu yetu kidogo.
Mchezo wa soka unahitaji sana subira na uvumilivu pia, hivyo inatupasa kwa sasa tumuache kwanza Mayanga atengeneze kikosi, inaonekana dhahiri Watanzania tuna papala na tunataka mafanikio kwa haraka haraka.
Imetokea kwa makocha wa Stars waliopita ambapo kila mmoja aliondolewa kwa sababu timu haifanyi vizuri bila kuangalia tatizo ni nini, tukianzia kwa Mbrazil, Marcio Maximo, Wadenishi, Jan Poulsen na Kim Poulsen, Mholanzi, Mart Nooij na mzalendo Charles Boniface Mkwasa "Master".
Makocha hao wote hawakudumu kutokana na matokeo ya Stars, maoni ya Watanzania ya kutaka wafukuzwe yalikuwa mengi mno, watu walikuwa wanataka ushindi tu hata kwakucheza na Brazil au Ivory Coast ambao wana mastaa wa kutosha wanaocheza barani Ulaya.
Nazikumbuka enzi za Maximo, Stars ilipata mafanikio kidogo ikiwemo kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, maarufu Chan, zilizofanyika nchini Ivory Coast.
Lakini Mbrazil huyo alitimuliwa baada ya kuingia kwa siasa za Usimba na Uyanga ndani ya TFF hasa kocha huyo anapofanya uteuzi wake wa wachezaji, kuna wadau walikuwa wakimshinikiza awaite wachezaji wanaowahusu wao, kocha huyo alibaki na misimamo yake na baadaye akafurushwa.
Kwa sasa inatupasa tumuache Mayanga aendelee na Stars yake kwani kipigo tulichokipata kimetoka kwa wanaojua mpira, huwezi kucheza na Ujerumani au Ufaransa halafu ukahoji kwanini tumefungwa, Algeria ni sawa na Ufaransa yetu au Ujerumani, na asiyekubali kufungwa wanasema si mshindani.
Kauli hiyo inafaa sana tukaiheshimu, nina imani kama tutaendelea kumuamini Mayanga na Stars yake kuna siku nasisi tutafurahia matunda yake, mwacheni aendelee kucheza na mataifa makubwa kisoka kama tulivyotaka, kufungwa ni sehemu ya kujifunza
ALAMSIKI