Khalfan Ngasa 'Babu': Unafahamu kwamba amemfunika mwanaye Mrisho Ngasa kwa rekodi Simba?



Na Prince Hoza

NAFURAHI umzima na unaendelea na majukumu yako ya kila siku huku ukiendelea kufuatilia safu yako pendwa ya 'Anayekumbukwa', kwa sasa habari ya mjini ni kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa kutumia BVR, nadhani ewe ndugu msomaji umejiandikisha.

Na kama ulikuwa haujajiandikisha ni vema ukaenda kupanga foleni ili ujiandikishe na utumie haki yako ya kidemokrasia kumchagua rais, mbunge na diwani wako katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Na huneda uchaguzi wa mwaka huu ukawa wa kihistoria hasa kutokana na Chama Cha Mapinduzi CCM kumpitisha ndugu John Pombe Magufuli kuwa mgombea wake wa urais, na aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa kuhamia Chadema ambapo naye huenda akasimishwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho kinachounda UKAWA.


Nimetumia muda mchache kuelezea masuala ya kisiasa, lakini ni kama tunakumbushana tu ili mradi shughuri zetu za kila siku ziende salama salmini.

Leo hii katika safu yetu hii namwelezea kiungo wa zamani wa Wekundu wa msimbazi Simba SC Khalfan Ngasa 'Babu', Ngasa alipata kuichezea klabu ya Simba mwishoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90.

Alifahamika zaidi kwa jina la Babu kutokana na umri wake kuwa mkubwa huku akiitumikia Simba SC kwa umahiri mkubwa, wengi watajiuliza Khalfan Ngasa ni nani?

Khalfan Ngasa 'Babu' ndiye baba mzazi wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simba na Azam FC Mrisho Ngasa ambaye kwa sasa anacheza soa la kulipwa nchini Afrika Kusini katika timu ya Free State Stars inayoshiriki ligi kuu.

Tofauti kati ya Mrisho Ngasa na baba yake mzee Khalfan Ngasa ni kwamba, Mzee Ngasa aliichezea Simba miaka ya 90 na Mrisho ameichezea Simba miaka hii ya 2000 na ndiyo maana vijana wengi wa sasa hawamfahamu Ngasa mkubwa ambaye ana rekodi za kutisha alipokuwa Simba SC.

REKODI ZA KHALFAN NGASA HIZI HAPA

Unaweza usikubaliane nami, lakini ukweli ndivyo ulivyo Khalfan Ngasa 'Babu' aliyesajiliwa na Simba akitokea Pamba FC ya Mwanza mwishoni mwa miaka ya 80 aliweza kuweka rekodi alipokuwa na Simba mwaka 1990 pale alipoiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi Daraja la kwanza Tanzania bara (sasa ligi kuu bara)

Ngasa mkubwa pia aliipa Simba ubingwa wa vilabu Afrika mashariki na kati sasa kombe la Kagame mwaka 1991 ilipofanyikia mjini Dar es Salaam, wakati hu Simba ilisheheni viungo wengi na hatari ambapo mkongwe huyo aliweza kung'ara mbele yao.

Mrisho Ngasa hakuweza kung'ara alipokuwa anaitumikia Simba

Ngasa mkubwa alisifika kwa uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira na pia alikuwa na kontroo ya hali ya juu, aliweza kupiga dana dana akiwa uwanjani na adui alishindwa kumpoka mpira, ni mahiri kwa chenga za maudhi, ana mashuti makali na mwenye nguvu.

Licha kwamba alionekana mkubwa kiumri na umbo, lakini aliwazidi vijana wengi aliokuwa akikutana nao uwanjani, Simba ilisheheni viugno wengi kama akina Bakari Idd, Ramadhan Lenny, Idd Seleman Kibode 'Nyigu', Method Mogella na wengineo lakini mkongwe huyo aliweza kutawala eneo la kiungo Simba.

Kiungo huyo mbali na kuiwezesha Simba kutwaa mataji mawili, moja likiwa la ligi kuu bara, na lingine la klabu bingwa Afrika mashariki na kati lakini aliiwezesha Simba kulitawala soka la Tanzania ndani na nje.

Simba ya wakati huo ilikuwa tofauti kubwa na hii ya sasa ambayo bado inasotea nafasi ya pili, Iko hivi! Mrisho Ngasa ambaye naye aliichezea Simba kwa msimu mmoja akitokea Azam FC hakuwahi kutwaa ubingwa wa bara wala kombe la Kagame ambalo zamani lilijulikana kama klabu bingwa Afrika mashariki na kati.

Hapo utaona kuna tofauti kubwa kati ya Ngasa mkubwa na mdogo, Ngasa mkubwa amepata mafanikio makubwa akiwa na Simba SC wakati Ngasa mdogo hakuweza kuisaidia Simba licha kwamba alipata bahati za kutakiwa na timu mbalimbali za nje na sasa ameangukia nchini Afrika Kusini.

Khalfan Ngasa aliibukia Pamba FC ya Mwanza ambayo alitamba nayo miaka ya 980 enzi hizo Pamba ilikuwa na nyota mbalimbali kama Msonga Rashid, Kitwana Seleman, Hamza Mponda, Ally Bushiri, Abdallah Bori, Saleh Mohamed, Fumo Felician, George Masatu, Hussein Marsha na wengineo.

Safu hii iliwahi kupata japo maelezo machache ya mkongwe huyo mwenye kuheshimika Simba akiwa na alama za vikombe viwili vikubwa ambapo aliwahi kusema kuwa yeye ni mnazi mkubwa wa Simba na si Yanga kama baadhi ya watu wanavyosema.

Ameongeza kuwa anapenda kumuona mwanaye (Mrisho) akifanikiwa zaidi kwenye soka kwani yeye ni mzazi ambaye pia amecheza soka, anadai mafanikio ya mwanaye pia yanamlenga na yeye.

Kikosi cha Simba cha zamani ambacho Ngasa mkubwa alikitumikia kwa mafanikio 

Ngasa mkubwa amefichua siri ya wachezaji wa zamani kujituma na kuzisaidia klabu zao pamoja na timu za taifa , ambapo amedai wachezaji wa zamani walijituma ili kuzipatia sifa klabu zao na si pesa kama ilivyo kwa wachezaji wa sasa.

Amedai si kwamba kwa sasa hakuna wachezaji wazuri kama ilivyo kuwa wao, 'Kwa sasa wapo wachezaji wazuri tena kuliko wa zamani isipokuwa wachezaji wa zamani watakabia kuwa wa zamani', alisema na kuongeza.

'Unajua wachezaji wa sasa wanachoangalia ni pesa tu, ndio maana utaona kuna ubinafsi kwenye timu, wachezaji hawajitumi kwa ajili ya timu ila anajituma ili apate pesa na umaarufu wa peke yake hapo utaona utofauti kati ya sasa na zamani ambapo sisi tulipigania timu yetu ili ipate kutambulika na ndio maana mnazikumbuka timu za zamani kama Pamba na nyinginezo', alisema Khalfan Ngasa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA