STARS YALAZIMISHWA SARE NYUMBANI

TANZANIA, Taifa Stars imeanza vibaya hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Msumbiji.

Katika mchezo huo, uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana, mabao ya Stars inayofundishwa na Mholanzi Mart Nooij yalifungwa na kiungo wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa.


Dakika 45 za kwanza zilimalizika bila bao na kipindi cha pili, Msumbiji walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 47 kwa penalti iliyokwamishwa nyavuni na Elias Pelembe baada ya Kevin Yondan kucheza rafu kwenye eneo la hatari. Mcha aliisawazishia Stars bao hilo dakika ya 65 akimalizia kazi nzuri ya Thomas Ulimwengu.

Mcha tena akaifungia Stars bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 71 kwa penalti, baada ya mabeki wa Mambas kumchezea rafu Mbwana Samatta kwenye eneo la hatari.

Stars iliongeza mashambulizi langoni mwa Msumbiji na kukosa mabao kadhaa ya wazi. Msumbiji walizinduka na kufanya shambulizi zuri lililowapatia bao la kusawazisha dakika ya 87 kupitia kwa Isaac Carvalho aliyetokea benchi pia.

Kwa matokeo, hayo Stars sasa itajitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele, au sare ya kuanzia mabao 3-3, wakati wenyeji wanaweza kunufaika na sare ya 1-1 au 0-0. Ikiwa 2-2 tena, mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Stars iliyofika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 1-0 nyumbani na sare ya 2-2 Harare, ikifanikiwa kuitoa Msumbiji itapangwa katika Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya Morocco mwakani.

Stars imekuwa ikinyanyaswa na Msumbiji miaka ya karibuni na mara mbili imewahi kutolewa na Mambas katika hatua za awali za AFCON. Kuwania Fainali za Ghana mwaka 2008, Stars ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ilifungwa 1-0 Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa kundi.

Kuwania Fainali za mwaka jana Afrika Kusini, Stars ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen, ilitolewa kwa penalti 5-4 na Msumbiji baada ya sare ya jumla ya 2-2.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mwinyi Kazimoto, Thomas Ulimwengu, Erasto Nyoni, John Bocco/Haroun Chanongo dk78, Mbwana Samatta/Simon Msuva dk83 na Mrisho Ngassa/Khamis Mcha dk57.

Msumbiji; Dario Khan, Momed Hagi, Zainadine Junior, Saddan Guambe, Francisco Mioche, Eduardo Jumisse/Isaac de Carvalho dk85, Elias Pelembe, Josemar Machaisse, Helder Pelembe, Almiro Lobo na Richard Campos.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA