ORIGI APIGIWA CHAPUO KUCHEZA LIGI KUU YA ENGLAND
Mchezaji wa zamani wa klabu ya Gor Mahia na timu ya taifa ya Kenya Haraambee Stars, Austin Oduor, amesema mshambuliaji matata wa timu ya taifa ya Ubelgiji Divorc Origi ameiva kucheza katika ligi kuu ya England.
''Asipoteze muda wake kwa sababu huu ndio umri mzuri kwake kushiriki ligi hiyo. Nitazungumza naye na babake baada ya kombe la dunia kwani singetaka tuanze kuzungumzia mengine wakati huu ila kombe la dunia tu.’’
Miongoni mwa timu za ligi kuu ambazo zimeonyesha nia ya kumsajili Origi ni Liverpool, Tottenham Hotspurs na Arsenal lakini kuna dalili Liverpool itamnasa kinda huyo ambaye alizaliwa Ubelgiji wakati babake Mike Okoth, raia wa Kenya, alipokuwa akicheza kandanda ya kulipwa nchini humo.
Origi mwenyewe anasema ana hamu sana ya kushiriki ligi kuu ya England bora apate klabu kitakachomfurahisha.
Babake Origi ni shabiki sugu wa Liverpool hivyo basi huenda akamshawishi mwanawe ajiunge na bingwa hao mara 18 wa ligi kuu ya England.
Lakini kabla mashindano ya kombe la dunia yaanze Okoth alisema atampa Origi uhuru wa kuamua ni klabu kipi anataka kuchezea England endapo atakiacha kile cha Ufaransa, Lille.