MAXIMO AMREJESHA NSAJIGWA YANGA

KOCHA mpya wa Yanga SC, Mbrazil Marcio Maximo amemrejesha beki wa zamani wa timu hiyo, Nsajigwa Joel Shadrack Mwandemele ‘Fusso’ katika timu hiyo.

Maximo alifanya kazi na Nsajigwa katika miaka yake minne ya kuifundisha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na alimpa Unahodha katika miaka yake miwili ya mwisho.

Hiyo ilifuatia kustaafu kwa Manahodha wake wawili wa awali, kwanza Mecky Mexime na baadaye Salum Swedi ‘Kussi’ na Nsajigwa aliendelea kuwa Nahodha wa Stars mbele ya kocha aliyemfuatia Maximo, Jan poulsen kabla ya kustaafu mwaka jana.


Na baada ya kurudi Tanzania kama kocha wa Yanga SC, Maximo amemkumbuka askari wake huyo wa zamani na kumrejesha Jangwani, ingawa safari hii harejei kama mchezaji, bali kocha.

Maximo amemrejesha Nsajigwa Yanga ili awe kocha wa kikosi cha vijana wa timu hiyo, maarufu kama Yanga B, wakati aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Salvatory Edward Augustino ‘Doctor’ anaingia kwenye benchi la ufundi la kikosi cha kwanza.

Maximo amevutiwa na utendaji wa kiungo wa zamani wa Yanga SC, Salva na ameona bora awe naye moja kwa moja kama Msaidizi wake wa kikosi cha kwanza na timu ya pili, iende kwa Nsajigwa.

Juma Pondamali ‘Mensah’ anaendelea kuwa kocha wa makipa, wakati Mbrazil mwingine, Leonardo Neiva anaendelea kuwa kocha Msaidizi Mkuu.

Yanga SC kwa sasa ipo kweye mazoezi makali, ikijiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao mjini Kigali, Rwanda.

Yanga SC inatarajiwa kuingia kambini Bagamoyo wakati wowote kwa maandalizi zaidi ya michuano hiyo, ambayo wamepangwa kundi A pamoja na wenyeji, Rayon Sport, KMKM ya Zanzibar, Coffee ya Ethiopia na Atlabara ya Sudan Kusini.

Kundi B lina timu za APR ya Rwanda, KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya Djibouti, wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.

Timu 14 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo kuanzia Agosti 8 hadi 24 mwaka huu- jumla ya mechi 34 zikichezwa katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo, Kigali.

Nsajigwa alikuwa Nahodha wa Stars wakati wa Maximo, hapa anakabiliana na Robinho katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Brazil

Rais Paul Kagame wa Rwanda ndiye mlezi wa mashindano haya ambaye hutoa dola za Kimarekani 60,000 kila mwaka kwa ajili ya zawadi.

Wizara ya Michezo ya Rwanda na mashirika mengine yatadhamini michuano hiyo, itakayokwenda sambamba na maazimisho ya miaka 20 ya mauwaji ya kimbau.

Televisheni ya kulipia ya Supersport ya Afrika Kusini ambao ni maswahiba wa muda mrefu wa CECAFA, ni miongoni mwa wadhamini pia na wataonyesha mechi zote za michuano hiyo moja kwa moja. Ratiba ya mashindano hayo inatarajiwa kutolewa wiki hii.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA