MAKALA: HUSSEIN SHARRIF CASSILAS KUSAJILIWA KWAKE SIMBA NA NDOTO YA KUWA TANZANIA ONE
JANA Simba SC ilifanya usajili wa wachezaji watatu kwa mkupuo, wamo walinda milango wawili ambao ni Hussein Sharrif 'Cassilas' na Peter Manyika mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa Manyika Peter Manyika.
Usajili huo ulienda sambamba na mchezaji mwingine aitwaye Hajibu, lakini usajili wa Cassilas ndio ulioweza kushtua zaidi hasa kutokana na ubora wake awapo uwanjani.
Cassilas ndiye kipa bora wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2013/14 akiwashinda walinda milango wote nchini, ligi ya bara imekuwa na changamoto zake katika suala la ushindani lakini Cassilas ameweza kuvuka.
Ligi kuu ya bara ilishirikisha makipa bora na mahiri lakini wote hawakuweza kufua dafu kwa Cassilas ambaye alikuwa anaiongoza Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro inayotumia uwanja wake wa Manungu.
Kati ya makipa walioshiriki ligi kuu bara ni pamoja na Juma Kaseja, Aishi Manula, Shaaban Kado, Ally Mustapha 'Barthez', Deogratus Munishi 'Dida', Ivo Mapunda na wengineo.
Cassilas anastahili pongezi kwa kufanikiwa kutajwa kipa bora nchini, uongozi wa klabu ya Simba chini yake Evans Elieza Aveva umeanza kazi kwa kishindo, kwanza ilianza kutembelea uwanja wa klabu hiyo uliopo Bunju, pili umeanza kufanya usajili.
Simba imekuwa na tatizo kubwa hasa katika sehemu ya mlinda mlango, mpaka ligi kuu ya bara inamalizika kilio kikubwa cha mwalimu wa timu hiyo Zdravko Logarusic ni mlinda mlango na beki wa kushoto.
Loga amekuwa akilalamika kuwa Simba inahitaji mlinda mlango mwingine wa kuweza kumletea ushindani kipa aliyepo Ivo Mapunda, Ivo Mapunda amekuwa akicheza peke yake kufuatia kutoridhishwa kwa udakaji wa Yaw Berko na chipukizi Abou Hashimu.
Hivyo Loga akapendekeza asajiliwe kipa mwingine, mawazo yalielekezwa kwa makipa wawili wa ndani ambao ni Ally Mustapha Barthez au Hussein Sharrif 'Cassilas'.
Hata hivyo mipango ya kumchukua Barthez ilishindikana kufuatia uongozi wa Yanga kumpa tena mkataba kipa wake Ally Mustapha 'barthez', awali Barthez alitangazwa kutemwa kutokana na kuifungisha Yanga ilipocheza na Simba katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara mzunguko wa kwanza Oktoba 20 uliochezwa uwanja wa Taifa ambapo Yanga na Simba zilitoka sare ya kufungana 3-3.
Matokeo hayo yaliwakera Wana-Yanga ambapo ikamlazimu Barthez kuchunguzwa na kutuhumiwa kuihujumu timu yake, Barthez alikuwa akipigiwa hesabu kurejea Simba lakini mipango hiyo ikashindikana.
Ndipo kamati ya usajili ya Simba ikiongozwa na Zakaria Hanspoppe na makamu wake Kassim Dewji 'Mzee wa fitina' walipoanza kuwania saini ya Cassilas.
Dili ilikamilika Alhamis ambapo mjumbe wa kamati ya usajili ya klabu hiyo Said Tully alipoweza kukamilisha kazi ya kumleta kipa bora wa ligi kuu bara Hussein Sharrif maarufu kama Cassilas.
Cassilas akiwa na mjumbe wa kamati ya usajili Said Tully baada ya kumwaga wino Simba.
Ujio wa Cassilas ndani ya Simba unaweza kutimiza ndoto za Loga kuwa na makipa wawili wenye uwezo unaofanana au kuzidiana, pia kuongezeka kwa kipa mwingine ambaye pia ni bora Peter Manyika kunaifanya Simba kukamilisha usajili wake wa makipa.
Hata hivyo mlinda lango Hussein Sharrif 'Cassilas' amefurahia ujio wake ndani ya Simba huku akisema ni furaha kwake, kujiunga Simba ni furaha katika maisha yake kwani aliwaza siku moja kuichezea timu hiyo.
Imekuwa ni bahati sana kwa mchezaji wa mpira wa miguu kupata nafasi ya kuchezea moja kati ya vilabu vikubwa na vikongwe nchini, hakutegemea kama atasajiliwa na Simba kwani licha ya kuipenda timu hiyo lakini ukubwa wa timu hiyo utamfikisha mbali.
Akizungumzia ndoto zake za kuwa Tanzania One, anasema sehemu pekee itakayomfanya kuzitimiza ndoto hizo ni Simba peke yake, ana imani kubwa atakuwa katika kikosi cha kwanza lakini amesema atapata ushindani mkubwa kutoka kwa makipa wenzake.
Amedai hatowaangusha mashabiki wa timu hiyo pindi tu akipata nafasi ya kucheza kwani anajua Simba ni timu kubwa na yenye mashabiki wengi kuliko aliyopata kuichezea ya
Mtibwa Sugar, pia ndoto zake za kucheza soka la kulipwa ughaibuni inaweza kutimia akiwa Simba.Umaarufu wa klabu hiyo nje ya mipaka ya Tanzania kunaweza kumfanya asajiliwe haraka, Mtibwa Sugar haijulikani nje ya nchi na ndio maana hakupata kusajiliwa nchini DRC-Congo licha ya kufuzu majaribio.
Lakini ukubwa wa timu ya Simba na ushawishi wake unaweza kumfanya apate maisha mapya ya soka na kufurahia kipaji chake, Cassilas anatajwa kama kipa bora kuliko hata Dida lakini alishindwa kuchaguliwa timu ya taifa kutokana na kutokuwa katika klabu kubwa nchini.
Ni suala la kusubiri kisha tuone, 0652 626627.