IVO MAPUNDA AMUHOFIA CASSILAS
Kipa chaguo la kwanza wa timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Ivo Mapunda, amesema kwamba anamhofia kipa mpya aliyetua kwenye kikosi hicho, Hussein Shariff 'Casillas' kutoka Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.
Casillas alisaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kuitumikia Simba mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili, Mapunda, alisema kwamba Casillas ndiye kipa bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita hivyo atajipanga kufanya mazoezi ili kulinda kiwango chake na kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza.
Mapunda ambaye aliwahi kuzichezea timu za Prisons ya Mbeya, Yanga ya jijini na St. George ya Ethiopia alisema kuwa hatabweteka na atahakikisha anapambana ili kulinda nafasi yake kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Cassilas ameanza kumtisha Mapunda baada ya kutua Simba akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro
Aliongeza kuwa kila mchezaji kwenye timu hana uhakika wa namba ndiyo maana wanapokuwa mazoezini wanajituma na kumshawishi kocha kuwapa nafasi.
"Casillas ni kipa bora msimu uliopita, hivyo ni mzuri na mimi nimejipanga kukabiliana na changamoto hiyo, pia naamini kila mmoja atahakikisha anamridhisha mwalimu," alisema kipa huyo.
Simba tayari imeshaanza kujifua kujiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Bara na jana jioni Mcroatia, Zdravko Logarusic, alikiongoza kikosi chake kwa mara ya kwanza tangu arejee kutoka likizo kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Mlimani.
Hata hivyo Simba kama zilivyo timu nyingine zenye wachezaji katika timu ya Taifa (Taifa Stars) itawakosa nyota wake wa kikosi cha kwanza katika maandalizi.
Nyota hao ni pamoja na Amri Kiemba, Haroun Chanongo, Jonas Mkude, Ramadhani Singano 'Messi' na Joram Mgeveke walio katika kambi ya timu ya Taifa Stars wakati Amissi ambwe naye ameitwa kwenye timu ya taifa ya Burundi huku baadhi wakiwa bado hawajaripoti mazoezini akiwamo beki, Donald Musoti.
Simba ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya nne na hivyo mwakani haitashiriki mashindano yoyote ya kimataifa wakati mabingwa ni Azam ambao watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Kagame huku Yanga walioshika nafasi ya pili watapeperusha bendera ya Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.