GOTZE ASEMA, LILE LILIKUWA BAO LA NGEKEWA TU KWAKE.

Shujaa wa Ujerumani, Mario Gotze amesema kufunga bao pekee na la ushindi katika fainali ya Kombe la Dunia ni kama bahati na zawadi yake katika msimu wake mgumu akiwa Bayern Munich.

Gotze (22), mwenye sura ya kitoto, alituliza kifuani mpira wa krosi ya Andre Schuerrle kabla ya kupiga shuti kufunga bao katika dakika ya 113, na kuipa Ujerumani ushindi 1-0 dhidi ya Argentina kwenye Uwanja wa Maracana, Rio de Janeiro, Brazil.


“Ni hisia ambazo siwezi kuziamini wala kuzielezea,” alisema kiungo huyo wa Bayern.

“Sijui hata nilielezee vipi hili. Unajikuta unafunga bao na hujui kitu kitakachotokea. Itakuwa ni sherehe pamoja na timu nzima na taifa kwa ujumla.  Ni kama ndoto iliyotimia.”

Gotze aliingia kuchukua nafasi ya mkongwe Miroslav Klose kabla ya kuanza kwa muda wa nyongeza. Hilo ni bao lake la 11 kuifungia timu ya taifa katika michezo 35 aliyoitumikia miamba hiyo maarufu kama ‘Die Mannschaft’.

Alitwaa pia tuzo ya mchezaji bora wa mechi, ambayo alipewa uwanjani hapo wakati Ujerumani ikiweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Bara la Ulaya kutwaa taji hilo katika ardhi ya bara la Amerika Kusini.

Gotze anaungana na ‘Der Bomber’ Gerd Mueller, ambaye alifunga bao la ushindi kwa Ujerumani Magharibi katika mchezo wa fainali 1974 mjini Munich, akiwa mchezaji mwingine wa Bayern kulipa ubingwa taifa hilo.

Gotze alitua nchini Brazil akiwa ametokea kwenye hali ngumu katika msimu wake wa kwanza na miamba hiyo ya Bavaria, akiwa ameshindwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha kocha Pep Guardiola.

Akiwa ametwaa mataji mawili ya Bundesliga na Borussia Dortmund, klabu ambayo alijiunga nayo akiwa na miaka nane, Gotze alikuwa adui namba moja wa mashabiki wa Borussia Aprili 2013, alipokubali uhamisho wa Euro 37 milioni ili kujiunga na Bayern.

Uhamisho huo umemfanya nyota huyo kuipa kisogo timu iliyomkuza na ya nyumbani kwao. Alikuwa nje katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei 2013, baada ya kuumia katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA