NDOTO za Yanga SC kwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zimeyeyuka leo licha ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie katika mchezo wa mwisho wa Kundi B usiku huu Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Yanga imezidiwa kete na AS FAR Rabat ya Morocco iliyomaliza na pointi tisa katika nafasi ya pili ya Kundi B, moja zaidi ya Yanga baada ya sare ya bila mabao na wenyeji, Al Ahly usiku huu Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo, Misri.
Mabao ya Yanga katika mchezo wa leo yamefungwa na mshambuliaji Muangola, Laurindo Dilson Maria AurĂ©lio ‘Depu’ la kwanza kwa penalti dakika ya 36 na la pili dakika ya 63, kabla ya beki Mkongo Chadrack Issaka Boka kufunga la tatu dakika ya 65.
Baada ya matokeo hayo, Al Ahly inamaliza kileleni mwa Kundi C na pointi zake 10, ikifuatiwa na AS FAR Rabat tisa na Yanga nane — wakati JS Kabylie inamaliza mkiani na pointi zake tatu.
