SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeziingiza kwenye ushindani mkali kampuni za michezo ya kubashiri baada ya kutangaza rasmi zabuni ya haki ya kubashiri mchezo wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba.
Mchezo huo unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi umepangwa kuchezwa Machi Mosi katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, na tayari umeanza kuonekana kama fursa muhimu ya kibiashara kwa sekta ya michezo ya kubashiri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, shirikisho limesema kuwa haki zote za kubashiri michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni mali ya TFF pamoja na washirika wake waliotambuliwa kisheria.
TFF imeeleza wazi kuwa kampuni yoyote ya kubashiri itakayojihusisha na kubashiri mchezo huo au michezo mingine ya ligi bila kuwa mshirika halali wa shirikisho hilo itakuwa imekiuka taratibu na sheria zilizopo.
Katika taarifa hiyo, shirikisho limetoa onyo kali kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni au taasisi yoyote itakayokaidi maelekezo hayo, ikiwa ni sehemu ya kulinda maslahi ya mpira wa miguu nchini na kuongeza uwajibikaji.
