Msemaji wa zamani wa klabu za Simba SC na Young Africans SC ambaye kwa sasa ni Diwani wa Kata ya Kariakoo Ndugu Haji S Manara amesema kwa kipindi alichoitumikia klabu ya Simba kama Msemaji wa timu hiyo hakuwa na ushabiki zaidi ya kazi.
Manara ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na kituo cha Crown FM ambapo amesema, "Yaani Mimi sio Yanga wa kubabaisha, Toka nazaliwa. Simba nlienda sababu ya kazi, hapa nina kadi za wana CCM wenzangu lakini nina kadi ya Young Africans" Alisema Manara akiongeza kuwa mashabiki wa Simba awali waliamini kuwa ni shabiki wa timu yao.
"Nina bahati moja, watu wa Simba wakati sijawa msemaji wa Simba, waliamini mimi ni mshabiki wao. Hali kadhalika na watu wa Yanga. Kabla sijawa msemaji wa Simba wala Yanga, walikuwa wanaamini mimi ni mtu wao kwasababu ya taaluma yangu" Alisema Manara akielezea taaluma ya baadhi ya waandishi wanaoonyesha mapenzi yao kwenye timu.
"Mi niko mwandishi ulikuwa hunikuti nafanya uchawa wa baadhi ya waandishi, kuonyesha mimi niko timu fulani. Sifanyi ujinga huo kabisa kabisa" Alisema Manara.
