Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Serikali yaidhinisha marekebisho ya katiba Simba


Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo imeridhia rasmi marekebisho ya Katiba ya Simba Sports Club, hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo, kuongeza uwazi wa umiliki na kufungua milango zaidi ya uwekezaji.

Akizungumza katika taarifa kwa vyombo vya habari, Msajili wa Vyama vya Michezo Nchini, Abel Mathias Nilangwa, alisema mchakato wa marekebisho hayo umehitimishwa kikamilifu baada ya kukamilika kwa hatua zote za kisheria na kiutawala, ikiwemo kukabidhi rasmi Katiba iliyoidhinishwa kwa uongozi wa klabu.

Nilangwa alisema hatua hiyo imefikiwa kufuatia maelekezo ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyetoa msisitizo mapema Februari kuhakikisha mchakato huo unakamilika kabla ya mwezi kuisha kwa maslahi ya klabu, wanachama wake na maendeleo ya michezo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Msajili, Simba ilianza mchakato wa mageuzi ya mfumo wake wa uendeshaji mwaka 2018 kwa lengo la kuruhusu uwekezaji. Hata hivyo, katika utekelezaji wake changamoto mbalimbali za kisheria na kiutawala zilijitokeza, zikiwemo masuala ya muundo wa umiliki, usajili wa wadhamini pamoja na uoanifu wa Katiba na matakwa ya taasisi za Serikali.

Marekebisho hayo yalijadiliwa na kupitishwa awali na Mkutano Mkuu wa Wanachama tarehe 30 Novemba, 2025, kabla ya kuwasilishwa Ofisi ya Msajili kwa ajili ya uhakiki. Rasimu ya kwanza iliwasilishwa Desemba 10, 2025 na kurejeshwa kwa maboresho, kabla ya Simba kuwasilisha tena rasimu iliyoboreshwa Desemba 24, 2025.

Baada ya kuombwa ufafanuzi wa baadhi ya vipengele Januari 5, 2026, klabu iliwasilisha toleo la mwisho Februari 5, 2026, hatua iliyofungua njia ya Serikali kufanya uchambuzi wa mwisho na kutoa idhini rasmi.

Nilangwa alisema Serikali imejiridhisha kuwa marekebisho hayo yanazingatia Kanuni za Msajili wa Vyama vya Michezo za mwaka 1999 na hayahatarishi usalama, hayavurugi amani miongoni mwa wanachama au jamii, wala kuathiri maendeleo ya klabu.

MABLRESHO MAKUU YA KATIBA

Miongoni mwa maboresho yaliyoidhinishwa ni kuanzishwa rasmi kwa Simba Sports Club Company Limited kama kampuni itakayoshughulikia shughuli za kibiashara na kiutendaji za klabu, huku umiliki wa hisa ukiwa wa ubia kati ya Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama na wawekezaji.
Katiba pia imeweka wazi kuwa:

Hisa za klabu zitamilikiwa kupitia Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama;
Baraza la Wadhamini litakuwa na wajumbe kati ya watano hadi saba;

Mkutano Mkuu unabaki kuwa chombo cha juu chenye mamlaka ya kuthibitisha au kumuondoa mjumbe wa Baraza la Wadhamini;

Angalau asilimia 51 ya hisa zitaendelea kumilikiwa na wanachama.

Serikali imeeleza kuwa muundo huu umeboreshwa ili kuendana na maamuzi ya Mkutano Mkuu, bila kubadili umiliki wa wanachama wala kuanzisha mfumo mpya.

Serikali yatuma wito kwa wanachama
Katika hitimisho lake, Msajili alisema Serikali haina jukumu la kuamua mfumo wa uendeshaji wa klabu, bali kuidhinisha marekebisho ya Katiba yanayokidhi sheria baada ya wanachama kufanya maamuzi yao.

Alitoa wito kwa wanachama wa Simba na wadau wa michezo kuheshimu maamuzi hayo ya kisheria ili klabu iendelee kusonga mbele kwa utulivu, mshikamano na mafanikio makubwa zaidi.

Kwa idhini hiyo, marekebisho ya Katiba ya Simba sasa yanatambuliwa rasmi na Serikali, huku klabu ikitarajiwa kuyatekeleza kwa kuzingatia kikamilifu Sheria, Kanuni na maamuzi ya Mkutano Mkuu kwa lengo la kulinda maslahi ya wanachama, wawekezaji na maendeleo ya michezo nchini.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya viwango vya ubora wa klabu barani, Simba ikiendelea kuwa juu ya klabu nyingine za Tanzania, nafasi ya tano. Orodha hiyo imetoka leo kuelekea droo ya hatua za awali za michuano ya klabu Afrika ambayo kwa mara ya kwanza kihistoria itafanyika nchini katika studio za Azam Tv, Tabata Jijini Dar es Salaam. Yanga ambayo kama Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa — yenyewe inashika nafasi ya 12, wakati timu nyingine katika orodha hiyo ni Namungo FC wanaoshika nafasi ya mwisho, ya 75 kwa pamoja na Salitas FC ya Burkina Faso, Ahli Benghazi ya Libya na NAPSA Stars ya Zambia. Kwa msimu ujao mbali na Simba na Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa, Azam FC na Singida Black Stars zitashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

Beno Ngassa mdogo wa Mrisho Ngassa anayekipiga Tanzania Prisons

Miongoni mwa viungo wa pembeni wanaofanya vizuri ni Benodict Khalfan Ngassa ambaye amekuwa akifanya vizuri. Ngassa ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba Jiji na Simba SC, Khalfan Ngassa, pia ni mdogo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simba na Azam, Mrisho Ngassa anatajwa ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kufanya makubwa siku za usoni. Mambo Uwanjani Blog itawaletea Makala maalum ya kiungo huyo hatari ambaye ndoto zake ni kufuata nyayo za kaka yake Mrisho Ngassa. Beno Ngassa