Na Prince Hoza Matua
DIRISHA dogo la Januari mwaka huu, Simba SC imefanya sajili mpya za wachezaji takribani saba ambazo zinalenga kuibadili timu hiyo katika mashindano mbalimbali inayoshiriki hapa nchini.
Miongoni mwa mashindano ambayo Simba inashiriki kikamilifu msimu huu ni pamoja na michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika ambapo timu hiyo ilikuwa inamalizia mechi zake kadhaa za hatua ya makundi ambapo msimu huu Simba iliangukia pua.
Wekundu hao wa Msimbazi, hawakuwa na msimu mzuri baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo, Simba iliyopangwa na timu za Esperance ya Tunisia, Petro de Luanda ya Angola na Stade Malien ya Mali.
Katika mechi za mzunguko wa kwanza, Simba ilijikuta inafungwa mechi zote, ikifungwa 1-0 na Petro de Luanda, 1-0 na Esperance na 2-1 na Stade Malien.
Wekundu hao wakaamua kufanya usajili mwingine baada ya ule wa Agosti mwaka jana kushindwa na kuleta mabadiliko, Simba imefanya usajili Ili angalau ifufue matumaini yake ya kutinga robo fainali kama ilivyozoea kufanya hivyo misimu kadhaa iliyopita.
Baada ya kufanya sajili hizo, Simba ilielekea katika mzunguko wa pili wa hatua ya makundi Ligi ya mabingwa Afrika, ikiwa na wachezaji wapya wakichangikana na wale wa zamani.
Simba ilipambana vilivyo na kuambulia pointi tano, Simba ilirudiana na Esperance na kutoka sare ya kufungana 2-2, sare nyingine ya 1-1 na Petro de Luanda na ushindi dhidi ya Stade Malien wa bao 1-0.
Licha kwamba Simba imeambulia nafasi ya mwisho na kuchangia kwake kushuka kwa nafasi mbili viwango vya CAF, lakini sajili za wachezaji wawili Alain Anicet Oura raia wa Ivory Coast na Labasse Gueye raia wa Senegal zinaweza kuwalipa.
Katika siku za karibuni, Simba imekuwa ikifanya usajili wa wachezaji wa kigeni mahiri, lakini zaidi imekuwa ikiwaimba wenyewe hasa viongozi, wanachama na mashabiki zake na si kundi la watu wa nje wasio karibu na Simba.
Mchezaji aliyekuwa akiimbwa sana ni Elie Mpanzu raia wa DR Congo na Jean Charles Ahoua raia wa Ivory Coast ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu bara.
Mpanzu safari hii si yule aliyekuwa akiimbwa, Ahoua naye hivyo hivyo, wawili hao wote wamejikuta wakisugua benchi, Ahoua aliyekuwa anatajwa kama MVP alisifika kwa kufunga magoli ya kutenga na kutoa assist, lakini msimu huu ajafunga hata bao moja wala kutoa assist.
Mpanzu naye amepotea kabisa kiasi kwamba mashabiki zake wakaanza kumuhusisha na Yanga, Mpanzu amekuwa akitajwa kujiunga na Yanga kiasi kwamba yeye mwenyewe hana furaha na timu yake ya Simba.
Siyo siri sajili mbili za Simba hasa za Gueye na Oura zimeonekana kuwa nzuri na huenda Simba ikarejea kwenye makali yake tuliyoyazoea, Gueye amekuwa akifunga mabao mazuri kwani ana uwezo wa kupiga mashuti ya kushtukiza, Gueye ni mchezaji mpambanaji na ana uwezo wa kuamua binafsi.
Sawa na Oura ambaye amekuwa tegemeo la Simba katika siku za karibuni Simba iliposhuka dimbani.
Mbali na Simba kufanya vema kwenye mechi za mzunguko wa pili wa Ligi ya mabingwa Afrika na kuambulia pointi tano, Simba inashiriki michuano ya kombe la CRDB, Ligi Kuu bara na mashindano mengine kama ya kombe la Mapinduzi na Muungano.
