Shirikisho la Kandanda barani Afirka CAF limetangaza michuano ya soka kwa mataifa ya Afrika mwaka 2027 itafanyika kama ilivyopangwa na ratiba kamili itatolewa hivi karibuni.
Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa CAF Patrice Motsepe alipozungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam ambako anahudhuria kikao cha kamati tendaji ya shirikisho hilo la mpira wa miguu. Motsepe amesema AFCON 2027 itakayoandaliwa kwa pamoja na mataifa matatu ya Kenya, Tanzania na Uganda itafanyika mwezi Juni au Julai.
Taarifa hiyo inazima minong´ono kuwa CAF huenda ingeipiga kalenda hadi mwaka 2028 kutokana na wasiwasi wa kutokamilika kwa maaandalizi. Tangazo la Motsepe litaongeza shinikizo kwa mataifa wenyeji kukamilisha haraka viwanja na miundombinu mingine inayohitajika kwa michuano hiyo.
