TIMU ya Yanga SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Yanga walitangulia kwa bao la beki wao wa kati, Ibrahim Hamad Abdullah ‘Bacca’ dakika ya 45’+1, kabla ya kiungo Aliou Dieng kuisawazishia Al Ahly dakika ya 60 akimchambua mchezaji mwenzake wa Mali, kipa Djigui Diarra.
Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha pointi tano katika mchezo wa nne, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu na Ahly wanaoongoza baada ya wote kucheza mechi nne.
Mechi nyingine ya Kundi B itafuatia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Jijini Rabat nchini Morocco — wenyeji, AS FAR Rabat wakimenyana na JS Kabylie ya Algeria.
Kuelekea mchezo huo, zote AS FAR Rabat na JS Kabylie kila moja ina pointi mbili baada ya mechi tatu za awali zikifuatana nafasi ya tatu na ya nne.
Ikumbukwe mechi zilizopita Yanga ilichapwa 2-0 na Al Ahly Uwanja wa Borg El Arab Jijini Alexandria na AS FAR Rabat ilitoka sare ya 0-0 na JS Kabylie Uwanja wa Hocine Aït Ahmed mjini Tizi Ouzou.
Mechi zijazo Yanga itaifuata AS FAR Rabat nchini Morocco kati ya Februari 6 na 8 na Al Ahly watakuwa wageni wa JS Kabylie Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Jijini Rabat.
