Baada ya takribani miaka 90 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936, Klabu ya African Sports ya Tanga imeandika historia mpya kwa kumiliki gari la wachezaji kwa mara ya kwanza, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo kongwe maarufu kama wana kimanumanu.
Mbali na gari hilo lenye thamani ya shilingi milioni 170, klabu hiyo pia imekabidhiwa msaada wa fedha taslimu shilingi milioni 30 kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abrahman Abdallah. Msaada wa kiasi kama hicho cha fedha pia umetolewa kwa Klabu ya Coastal Union.
Mashabiki wa African Sports wamesema umiliki wa gari hilo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kukodisha usafiri kwa ajili ya michezo, hasa katika kipindi ambacho klabu inapanga kupanda daraja msimu ujao, huku wadau wa soka wakihoji ni klabu gani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo hadi leo bado haijawahi kumiliki gari lake la wachezaji.







