Mshambuliaji Jonathan Sowah amefunguka kwa majonzi, akieleza kosa analolijutia zaidi katika taaluma yake ya soka tukio linalosema bado linamwathiri kisaikolojia hadi leo.
Sowah amesema aliwahi kuwa na ndoto ya kuichezea Yanga SC, ndoto iliyojengwa kupitia uhusiano wake wa karibu na Eng. Hersi Said, ambaye anamchukulia kama mzazi kutokana na mchango wake mkubwa tangu akiwa Medeama.
Ndoto hiyo ilizidi kuimarika baada ya kuvutiwa na mapokezi ya mashabiki wa Yanga alipofika Dar es Salaam. Hata hivyo, baada ya kukosa mwendelezo wa mawasiliano, alikubali kujiunga na Singida Black Stars kwa ushauri wa Hersi, akiamini ingetumika kama daraja.
Mambo yalibadilika baada ya kupata ofa ya Simba SC, aliyoichagua kwa sababu za kujitangaza kimataifa. Tukio analolijutia zaidi ni kuchana picha ya Rais wa Yanga wakati wa utambulisho wake Simba akitaja kuwa hakufanya kwa hiari bali kwa shinikizo la mazingira.
Kwa unyenyekevu, Sowah ameomba radhi kwa Eng. Hersi Said, akisisitiza bado anamheshimu kama mzazi na anaamini amani ya moyo ndiyo itakayomrudisha kwenye ubora wake wa kufunga mabao.
