Simba amekamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Mofossé Trésor Karidioula, katika dirisha dogo la usajili kwa ajili ya msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara Na Mashindano Ya kimataifa.
Karidioula, mwenye umri wa miaka 27, amejiunga na kikosi cha simba huku akiwa na rekodi ya kucheza katika ligi mbalimbali za Afrika na uzoefu wa kimataifa.
Mchezaji huyo aliitumikia klabu ya Haras El Hodood ya Misri msimu uliopita kabla ya kuwa huru, na sasa anaendelea na safari yake mpya akiwa Simba. Kabla ya kuichezea Misri, Karidioula alionyesha ubora wake akicheza kwa vilabu kama Williamsville AC na ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Simba wamemsajili akitokea Marumo Gallants FC ya Afrika Kusini.
Karidioula anacheza katika nafasi za mbele kama winger au mshambuliaji, akijulikana kwa kasi yake, mbinu bora ya kuvunja safu za ulinzi na uwezo wa kufunga na kusaidia mabao. Uzoefu wake mkubwa uwanjani unatarajiwa kuongeza nguvu kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Simba, huku akiwa amevaa jezi nambari 77.
Kocha na uongozi wa Simba wanamwona Karidioula kama kiungo muhimu katika mipango ya klabu kushindana vyema ndani ya ligi na mashindano ya kimataifa msimu huu. Usajili wake umeongeza chachu na matumaini kwa mashabiki wa klabu hiyo kuwa msimu huu utaisha kwa mafanikio makubwa.
