KIPA wa zamani wa Kimataifa wa Tanzania, Manyika Peter Manyika (52) amefariki dunia Alfajiri ya leo Jijini Dar es Salaam.
Manyika ambaye ni baba wa kipa wa zamani wa Simba SC Peter Manyika Junior - mwili wake umehifadhiwa katika hospital ya Mwananyamala, Dar es Salaam huku taratibu za mazishi zikiendelea.
Manyika aliibukia klabu ya Mtibwa Sugar akiipandisha Ligi Kuu mwaka 1996, kabla ya kuhamia Sigara FC ya Dar es Salaam ambako alidumu kwa msimu mmoja, 1997.
Akiwa Sigara aliiponza timu hiyo kushushwa Daraja baada ya kupokwa pointi za mechi zote alizodaka kwa sababu ya ukiukwaji wa taratibu za usajili wake kutoka Mtibwa Sugar.
Mwaka 1998 alijiunga na Yanga SC ambako aliidakia hadi mwaka 2001 alipokwenda Botswana kucheza soka ya kulipwa hadi mwaka 2004 akarejea nchini na kwenda kujiunga tena na Mtibwa Sugar alikocheza hadi mwaka 2006 alipostaafu.
Manyika pia alikuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kati ya mwaka 1998 na 2002 alipopokonywa namba na Juma Kaseja.
Baada ya kustaafu soka, pamoja na Ukocha lakini pia Manyika alikuwa anajishughulisha na muziki.
