Na James Shabay
Katika historia ya soka la Tanzania, yapo majina mengi yaliyopitia viwanjani, lakini ni machache sana yanayostahili kuitwa magwiji.
Miongoni mwa majina hayo ni Kenneth Mkapa, mchezaji wa zamani wa Young Africans Sports Club (Yanga SC) na Taifa Stars, ambaye mchango wake hauwezi kufutwa na muda.
Mkapa alikuwa mchezaji mwenye nidhamu, akili ya mchezo, na uwezo mkubwa wa kuongoza wenzake uwanjani.
Akiwa na jezi ya Yanga SC, alitoa kila alichonacho kwa ajili ya nembo ya klabu, akijenga taswira ya mchezaji anayeheshimu jezi na mashabiki.
Vilevile, alipovaa jezi ya Taifa Stars, aliwakilisha taifa kwa moyo wa kizalendo, akipambana kwa hali na mali kuitangaza Tanzania kimataifa.
Hata hivyo, pamoja na mchango huo mkubwa, bado kuna swali linalobaki vichwani mwa wadau wengi wa soka: kwa nini gwiji kama Kenneth Mkapa hapewi heshima kubwa inayostahili katika mpira wetu?.
Ni nadra kumuona akitajwa kwenye mijadala mikubwa ya kihistoria ya soka letu, hafikiwi mara kwa mara katika hafla rasmi, na simulizi za mafanikio yake hazipewi uzito unaolingana na mchango wake.
Umuhimu wa Kenneth Mkapa hauishii tu kwenye kile alichofanya akiwa mchezaji. Hata baada ya kustaafu soka, bado amebaki kuwa kioo cha kuigwa kwa wachezaji chipukizi mfano wa nidhamu, unyenyekevu na mapenzi ya kweli kwa mchezo.
Ni aina ya watu ambao uzoefu wao ungeweza kutumika zaidi katika kuijenga kesho ya soka letu, endapo wangetambuliwa na kuhusishwa ipasavyo.
Soka hukua kwa kuheshimu historia yake. Kuwapa thamani magwiji wetu siyo hisani, bali ni wajibu. Kenneth Mkapa anastahili heshima kubwa zaidi, kutambuliwa waziwazi, na kuenziwa kama sehemu muhimu ya safari ya soka la Tanzania.
Kwa kufanya hivyo, tunawaheshimu waliotutangulia na wakati huo huo tunawaonesha vijana wetu kuwa jitihada, nidhamu na uzalendo vina thamani ya kudumu.

