Klabu ya JS Kabylie imekamilisha usajili wa kiungo chipukizi Ecua Celestin (24) kwa mkopo akitokea klabu ya Young Africans SC (Yanga) katika dirisha dogo la usajili linaloendelea kwa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, Ecua Celestin tayari ameshakamilisha taratibu zote muhimu ikiwemo makubaliano ya kimkataba, vipimo vya afya pamoja na vigezo vya kiufundi, hivyo anatarajiwa kuanza mara moja majukumu yake mapya na klabu hiyo kwa kipindi cha mkopo.
Usajili wa Celestin unaonekana kuwa ni sehemu ya mkakati wa JS Kabylie Africans kuimarisha kikosi chao kuelekea michezo ya ushindani iliyopo mbele, huku wakihitaji nguvu mpya katika eneo la kiungo chenye uwezo wa kucheza kwa kasi, nguvu na akili ya mchezo. Uongozi wa klabu hiyo unaamini kuwa ujio wa Celestin utaongeza ushindani ndani ya kikosi na kuleta ubora zaidi katika safu ya kati.
Kwa upande wa Young Africans SC, hatua ya kumtoa Celestin kwa mkopo imeelezwa kuwa ni mpango wa kumpa mchezaji huyo nafasi ya kupata dakika zaidi za kucheza, uzoefu wa kimataifa pamoja na kukua kiuchezaji, jambo litakalomsaidia kurejea akiwa mchezaji bora zaidi hapo baadaye.
