Na Prince Hoza Matua
KLABU ya Simba SC imemtambulisha beki wa kushoto, Nickson Clement Kibabage (25) kuwa mchezaji wake mpya akijiunga na klabu hiyo kutoka Singida Black Stars.
Kibabage alijiunga tena na Singida Black Stars msimu huu akitokea Yanga alikodumu kwa misimu miwili kati ya mwaka 2023-2025.
Alikwenda Yanga SC akitokea Singida Black Stars ambako awali alicheza kwa msimu mmoja akitokea KMC ambako alikuwa anacheza kwa mkopo kutoka Difaâ Hassani El Jadidi ya Morocco.
Kibabage alijiunga na Difaâ Hassani El Jadidi mwaka 2019 akitokea Mtibwa Sugar iliyomuibua katika timu yake ya vijana na kufanya vizuri kikosi cha kwanza msimu mmoja tu, 2018-2019 kabla ya kuuzwa Morocco kwa mkataba wa miaka minne.
Ujio wake kwenda Simba, umezua sintofahamu nyingi hasa kutoka kwa mashabiki wengi wakiwa ni wa Yanga SC ambapo wanabeza usajili huo, inaonekana Simba imefulia kiasi kwamba inashindwa kuingia sokoni kutafuta beki mwenye uwezo mkubwa wa kucheza beki ya kushoto.
Tangu alipoondoka Mohamed Hussein Tshabalala au Zimbwe Jr aliyejiunga na Yanga, Simba inaonekana kushindwa kupata mlinzi mwingine wa kushoto hadi kuangukia kwa Kibabage.
Baada ya kuondoka Tshabalala, uongozi wa Simba ulikamilisha usajili wa beki mwingine wa kushoto Anthony Mligo kutoka klabu ya Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi.
Mligo lilikuwa chaguo la kocha wa klabu hiyo Fadlu David's ambaye kwasasa ameondoka kwenye klahu hiyo na kocha wa sasa Steve Barker ajafurahishwa na kiwango chake na ametoa pendekezo asajiliwe beki mwingine wa kushoto.
Barker ameuagiza uongozi wa Simba umsajilie mabeki wawili wa kushoto mmoja akiwa ni mzawa na mwingine wa kigeni, hapo ndipo viongozi wa Simba walipoona umuhimu wa kumsajili Kibabage, kwani wanasema hakuna beki mzawa wa kushoto kama Kibabage.
Ni kweli kwamba Yanga walimtema kwa sababu wanao mabeki wawili ambao ni bora, Chadrack Boka raia wa DR Congo na mzawa Mohamed Hussein Tshabalala walitosha kumuondoa Kibabage kwenye kikosi cha Yanga.
Simba kuamua kumsajili Kibabage siyo dhambi na wala siyo kosa, kwani hata Yanga wamewahi kuwasajili wachezaji waliotemwa na Simba na waliweza kupokelewa vema na mashabiki wao.
Wanasimba wasiwe wanyonge kubezwa kwa Kibabage, kwani Simba siyo timu ya kwanza kufanya hivyo, Yanga iliwahi kumsajili Amisi Tambwe ambaye aliachwa na Simba, pia ikamsajili Jean Baleke ambaye naye aliwahi kuachwa na Simba.
Lakini haitoshi Yanga wakaendelea kusajili wachezaji wanaotemwa na Simba, kwani walimsajili Augustine Okrah, ninaamini kabisa Nickson Kibabage ni mchezaji mzuri na ataendelea kukiwasha kwenye kikosi cha Simba msimu aliojiunga nao.
ALAMSIKI
