Serikali kupitia Baraza la michezo imetoa maelekezo Katiba mpya ya Simba SC inapaswa kumtambua M/Kiti wa Klabu kuwa ndiye M/Kiti wa Bodi ya Wakurugenzi maana klabu ina umiliki mkubwa ( 51%) na wawekezaji (49%).
Serikali inataka kuwe na wawekezaji kuanzia watatu.
Serikali imetaka Katiba ifanyiwe maboresho ya kutamka bayana kuwa Mwenyekiti wa Simba Sports Club ndiye Kiongozi Mkuu wa Chombo cha Utawala ndani ya Klabu na hivyo awe na mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu wa wanachama kwa kuwa masuala yanayojadiliwa juu ya uanachama na maendeleo ya Klabu yanaathiri moja kwa moja maslahi ya wanachama.
Mwenyekiti wa Klabu huyo ndiye awe Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Sports Club Company Limited kwa kuzingatia kuwa wanachama kupitia Klabu ndio wenye umiliki wa hisa nyingi (51%) na hivyo viongozi wote walio chini ya Katiba ya Klabu watawajibika kwake katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, Katiba na kanuni zinazoongoza Klabu.
Serikali pia imetaka kurekebishwa kwa matumizi ya neno "MWEKEZAJI" ndani ya rasimu ya Katiba na badala yake itumike dhana pana ya "WAWEKEZAJI" na iweke bayana kuwa Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama, ndilo litakaloingia mikataba na makubaliano yoyote na wawekezaji.
Marekebisho haya yanakusudia kupanua wigo wa uwekezaji wa kibiashara ndani ya Klabu kwa maendeleo ya Klabu na ulinzi wa maslahi ya wanachama kama wamiliki halali wa Simba Sports Club.
