WENYEJI, Pamba Jiji FC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Mabao yote ya ‘Wana Kawekamo’ jioni leo yamefungwa na mshambuliaji Mkenya - Mathew Tegisi Momanyi dakika ya saba na 26 na kwa ushindi huo – Pamba Jiji inafikisha pointi 15 na kupanda tena kileleni, wakiizidi pointi mbili JKT Tanzania baada ya wote kucheza mechi nane.
Kwa upande wao, KMC hali inazidi kuwa mbaya baada ya kupoteza mchezo wa sita leo, wakiwa wametoa sare moja na kushinda moja kati ya nane walizocheza, hivyo wanabaki na pointi zao nne wakiendelea kushika mkia katika ligi ya timu 16.

