TIMU ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza Raundi ya Pili kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika Wanawake 2026 nchini Morocco jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Twiga Stars inayofundishwa na kocha Bakari Nyundo Shime yamefungwa na washambuliaji Aisha Juma Mnunka wa Simba Queens dakika ya 23 na Jamila Rajab Doxa wa JKT Queens dakika ya 56.
Ethiopia inayofundishwa na Kocha Mkuu, Yosef Gebrewold itaikaribisha Tanzania Oktoba 28 katika mchezo wa marudiano Uwanja wa Abebe Bikila Jijini Addis Ababa kujaribu kupindua matokeo na mshindi wa jumla atafuzu WAFCON 2026 inayotarajiwa kuanza Machi 17 hadi April 3 mwakani.
Twiga Stars imewahi kucheza Fainali za WAFCON mara mbili tu, 2010 nchini Afrika Kusini na 2024 nchini Morocco na mara zote wakitolewa katika hatua ya makundi.