TIMU ya Simba SC imefanikiwa kuingia Hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya sare ya 0-0 na Nsingizini Hotspur ya Eswatini katika mchezo wa marudiano Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Simba inanufaika na ushindi wa 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspur kwenye mchezo wa kwanza mabao ya beki mpya, Wilson Edwin Nangu dakika ya 45’+1 na kiungo mshambuliaji, Kibu Dennis Prosper mawili dakika ya 82 na 90’+1 Oktoba 19 Uwanja wa Taifa wa Somhlolo nchini Eswatini.
Simba SC inaungana na watani wao wa jadi, Yanga SC kutinga hatua hiyo ya makundi inayoshirikisha timu 16 – wakati katika Kombe la Shirikisho pia timu zote mbili za Tanzania zimeingia hatua ya makundi pia, Azam FC na Singida Black Stars.
Droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika itapangwa Jumatatu ya Novemba 3 katika studio za SuperSport Jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambao ni washirika wa Matangazo wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuanzia Saa 7:00 mchana.
