Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imempa jukumu Cedrick Kaze kuinoa timu hiyo hadi mwishoni mwa msimu kufuatia uamuzi wa kuachana na Kocha wake Mkuu, Nasreddine Nabi jana.
Kaze kabla ya kubebeshwa jukumu hilo la kukaimu nafasi ya Ukocha Mkuu, alikuwa kocha msaidizi katika kikosi hicho, nafasi ambayo aliipata kutokana na kupendekezwa na Nabi.
Taarifa iliyotolewa na Kaizer Chiefs imefafanua kwamba Kaze ataiongoza timu hiyo kwa kushirikiana na Khalil Ben Youssef.
"Kufuatia taarifa ya kuachana kwa makubaliano baina ya Kaizer Chiefs FC na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, klabu inathibitisha kwamba makocha Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze, wataongoza benchi la ufundi kwa kipindi chote kilichobakia cha msimu.
"Usimamizi wao utahakikisha muendelezo na uimara wakati klabu ikiendelea kujiandaa na mechi zijazo za ndani na ya bara," imesema taarifa ya Kaizer Chiefs.