BEKI wa zamani wa kushoto wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Modest Pambamotosapi (55) amefariki dunia jioni ya leo majira ya Saa 1:40 usiku nyumbani kwao, Mtaa wa Kisangani mjini Kigoma.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu usiku huu kutoka Kigoma, baba mzazi wa Alphonce – Mzee Modest Pambamotosapi amesema kwamba taratibu za mazishi zitafanywa kesho na siku ya mazishi yake itatajwa.
Alphonce amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, maradhi ambayo yalikatisha Maisha yake ya soka katika klabu ya Mtibwa Sugar.
Mzee Modest amesema kijana wake ameacha watoto watatu ambao yeye anawafahamu na wote wanajitegemea kwa sasa - Tabu na Kelvin wapo Dar es Salaam na mdogo wao, Rachel ambaye yupo Arusha.
Modest aliibukia Pamba FC ya Mwanza mwaka 1993 ambayo ilimtoa SUA ya Morogoro ikiwa Ligi Daraja la Pili, sasa Championship, baada ya awali kuchezea timu za Halmashauri na NBC za kwao, Kigoma.
Alijiunga na Simba SC mwaka 1995 ambako alicheza hadi mwaka 1998 akajiiunga na Yanga kwa mkopo kwa ajili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika – lakini baada ya michuano hiyo akatimkia Botswana ambako alichezea timu ya Jeshi la nchini hiyo, BDF.
Mwaka 2001 alirejea nchini na kujiunga na Mtibwa Sugar ambayo aliichezea hadi mwaka 2006 alipolazimika kustaafu baada ya kuanza kusumbuliwa na maradhi.
Modest amekuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania tangu mwaka 1994 akijivunia kushinda mataji ta Kombe la CECAFA Challenge mwaka 1994 nchini Kenya na Kombe la CECAFA Castle mwaka 2001 Jijini Mwanza.
Mungu ampumzishe kwa Amani. Amin.