TIMU ya Singida Black Stars imeanza vyema Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, KMC FC leo Uwanj wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, beki Muivory Coast, Tra Anthony Urbain Tra Bi dakika ya 35 ya mchezo huo.
Ushindi huo kwa Singida Black Stars ni sawa na mwendelezo wa ubabe wa Kocha Muargentina, Miguel Gamondi kwa mpinzani wake wa Brazil, Marcio Maximo wa KMC.
Ikumbukwe Septemba 13 Singida Black Stars iliichapa KMC FC 2-0 katika mchezo wa Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame hapo hapo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Wote wawili, Gamondi na Maximo ambao ni makocha wa zamani wa klabu ya Yanga - wamejiunga na timu hizo msimu huu.