TIMU ya JKT Queens imefanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa ya Wanawake Afrika Mashariki na Kati ya CECAFA baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda katika mchezo wa Fainali leo Uwanja wa Moi International Sports Centre uliopo Kasarani Jijini Nairobi nchini Kenya.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, kiungo chipukizi wa umri wa miaka 17, Winfrida Hubert Gerald dakika ya tano na hilo linakuwa taji la pili la michuano hiyo kwao baada ya lile walilotwaa mwaka 2023 nchini Uganda.
JKT Queens inajikatia tiketi ya kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, michuano itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Algeria.
Pamoja na kutwaa taji hilo, JKT Queens imetoa Mfungaji Bora ambaye ni mshambuliaji wake, Jamila Rajab aliyefunga mabao matano, akifuatiwa kwa mbali na wachezaji watatu wa Kampala Queens, Kamiyati Naigaga, Tourist Lema Tone, Peace Muduwa na Emily Kemunto wa Police Bullets na Winfrida Mathias wa JKU Princess waliofunga mabao mawili kila mmoja.
Mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, bao pekee la mshambuliaji Mganda, Margaret Kunihira limewapa wenyeji, Police Bullets Medali ya Shaba baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Kampala Queens ya Uganda hapo hapo Uwanja wa Moi Kasarani.
Ikumbukwe JKT Queens iliingia Fainali baada ya kuwatoa wenyeji, Police Bullets kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 na Rayon Sports iliifunga Kampala Queens kwa penalti pia, 4-2 kufuatia sare ya bila mabao ndani ya dakika 120 mechi hizo zote pia zilipigwa hapo hapo Moi.