“Goli la Pacome limeibua mjadala mkubwa. Mashabiki wengine wanalia offside, wengine wanashangilia bila kuuliza. Hebu tuweke hisia pembeni, tuzungumze sheria.
Pacome kweli alikuwa kwenye nafasi ya offside awali. Lakini kumbuka, offside siyo kusimama tu mbele ya beki, ni kuhusika moja kwa moja kwenye mchezo. Pale alipokuwa amesimama hakugusa mpira, hakumkwaza beki, hakuzuia kipa kuona. Kwa lugha ya kanuni – ‘not interfering with play’.
Mpira ulipoenda kwa Maxi, ndipo mchezo ukaendelea. Pacome akajitoa nyuma, akarudi sambamba na mabeki. Kipa Camara alipookoa, Pacome hakuwa tena yule aliye kwenye offside awali. Akawa ‘legal’. Ndiyo maana bao likaonekana safi.
Kwa kifupi, wale wanaopiga kelele za offside wanapaswa kusoma tena Law 11. Sheria haipo kwa hisia, ipo kwa tafsiri sahihi. Goli ni halali.
Kitu cha msingi cha kujifunza hapa – makocha na mabeki wanatakiwa kuwa makini zaidi, maana washambuliaji wa aina ya Pacome wana akili za mbio kuliko sheria inavyoruhusu. Huyu kijana hajaja kwa masihara.”