TIMU ya Singida Black Stars imefanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Hilal Omdurman ya Sudan leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Singida Black Stars inayofundishwa na Kocha Muargentina, Miguel Angel Gamondi yamefungwa na kiungo wa Kimataifa wa Zambia, Clatous Chota Chama dakika ya 20 na 57, wakati bao pekee la Hilal Omdurman limefumgwa na kiungo wa Kimataifa wa Sudan, Abdelrazig Yagoub Omer Taha dakika ya 31.
Chama ambaye amejiunga na Singida Black Stars mwezi uliopita akitokea Yanga alikodumu kwa misimu miwili baada ya awali kuchezea Simba SC kwa muda mrefu alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi hiyo ya Fainali na kuzawadiwa Sh. 500,000.
Hilo linakuwa taji la kwanza kabisa katika historia ya Singida Black Stars, huku Gamondi akiendeleza rekodi yake nzuri ya kuzipa mataji timu kama ilivyokuwa wakati anafundisha Yanga.
Mapema katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, bao pekee la kiungo Mburkinabe, Raouf Memel Dao dakika ya 45 limeipa APR FC ya Rwanda ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, KMC FC hapo hapo Uwanja wa KMC Complex.