Na Prince Hoza Matua
KILA Mwanayanga aliyeona jina la Azizi Andabwile katika mechi hiyo ya watani wa jadi basi lazima alishtuka na kuogopa na wengine walifikia stage ya kuhoji huyo kwanini aanze lakini mwamba akaja kuwaziba midomo kwa performance bora sana.
Kiukweli mwamba kauwasha sana tena sana anafaa kuwa Man of match, lakini cha ajabu tangu mwanzo mwa mechi hadi mwishoni huku katika kibanda umiza kuna watu walikuwa wanapiga kelele wanataka atolewe sasa sijui walikuwa wanaangalia mechi tuliokuwa tunaangalia sisi au marudio.
Ujio wa kocha Roman Folz raia wa Ufaransa mwenye asili ya Morocco, umeweza kubadili upepo ndani ya kikosi cha Yanga SC msimu huu na Azizi Andabwile amechukua hatami.
Maisha ya Andabwile ni ya kupanda na kushuka, alijiunga na Yanga kimaajabu, kwani wakati anang' ara kwenye soka, hakupata nafasi ya kusajiliwa na klabu yoyote kubwa kati ya Yanga au Simba.
Mchezaji huyo aliibuliwa na timu ya Mbeya City ya mkoani Mbeya, mkoa ambao ndiko alikotokea, wakati mashabiki wengi wa soka nchini wakiamin kwamba nafasi yake ya kucheza vilabu vikubwa vitatu vya Yanga, Simba au Azam ilikuwa wakati ule, lakini bahati yake imechomoza jioni.
Andabwile ni kiungo mkabaji anayeweza kucheza vizuri namba sita, alipotea ghafla kwenye soka kabla ya Singida Black Stars kumrejesha hewani na akaanza kuchomoza upya.
Msimu uliopita Singida Black Stars walimpeleka kwa mkopo Yanga SC, ingawa hakupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, maisha yake ndani ya Yanga hayakuwa mazuri kwani benchi lilimtesa.
Yanga iliyonolewa na makocha tofauti akianza na Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina, Sead Ramovic raia wa Ujerumani na Miloud Hamdi raia wa Algeria, wote hawakumpa nafasi kutokana na ubora wa Khalid Aucho.
Ni ngumu kwa kocha yoyote kumuweka nje Aucho na kumfikiria Andabwile, mchezaji huyo aliendelea kukaa benchi hata kama Aucho hachezi, kwakuwa Yanga ilikuwa na namba sita mwingine Jonas Mkude ambaye naye alikuwa na kiwango bora.
Licha ya nyota hao wawili, Aucho na Mkude) kuondoka kwenye kikosi hicho, kuelekea mchezo wa dabi, Yanga na Simba kuwania Ngao ya Jamii, jina la Duke Abuye lilikuwa linatajwa kwenye namba sita.
Wachambuzi wengi wa soka walienda na jina la Duke wakidhanj Kwamba ataanza kwenye kikosi hicho akichukua nafasi ya Aucho, lakini ndivyo sivyo, kocha Roman Folz alimwanzisha Andabwile.
Roman alianza kumuamini Andabwile tangia alipoanza kukinoa kikosi cha Yanga mwanzoni mwa msimu huu akichukua mikoba ya Miloud Hamdi, Andabwile aliaminiwa kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifal dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda mchezo uliofanyika uwanja wa Amahoro mjini Kigali.
Katika mchezo huo Yanga SC ikishinda mabao 3-1, Andabwile alijifunga, lakini mashabiki wa Yanga walimsamehe wakiamin kwamba kujifunga kwake kulitokana na kukaa kwake benchi muda mrefu hivyo kulimuondolea kujiamini.
Lakini Folz aliendelea kumuamini kwenye mechi nyingine za kirafiki, kwenye mchezo wa watani hakuna aliyedhani kama Folz atamuanzisha kwani historia ya mechi hiyo kila timu hupanga wachezaji wanaoaminika, mimi mwenyewe nilijua Duke ataanza kama namba sita wa moja kwa moja.
Kwa jinsi alivyocheza kwenye mchezo huo na timu yake ikishinda, sidhani kama kocha atamweka nje katika michezo ijayo, tutegemee kimuona Andabwile kwenye mchezo dhidj ya Willete ya Angola.
ALAMSIKI